Ombi la Bangladesh kwa UN kuhusu Waislamu wa Rohingya
-
Waziri Mkuu wa Bangladesh, Bi Sheikh Hasina Wazed
Serikali ya Bangladesh imeutaka Umoja wa Mataifa kutenga eneo maalumu litakalokuwa chini ya umoja huo kwa ajili ya kuwadhaminia usalama Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaouliwa kikatili na mabudha wa Myanmar.
Waziri Mkuu wa Bangladesh, Bi Sheikh Hasina Wazed amesisitiza hayo pambizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini News York Marekani na kuongeza kuwa, serikali ya Myanmar inapaswa kukubali bila ya masharti yoyote kukomesha mauaji dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na uangamizaji wa mbari unaofanywa na mabudha wenye chuki za kidini katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo. Vile vile ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka za kukomesha mgogoro wa wakimbizi wa Waislamu hao.
Aidha amemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutuma haraka maafisa wa umoja huo kwa ajili ya kwenda kuwalinda kikamilifu raia wanaoangamizwa kinyama na mabudha makatili huko Myanmar.
Waziri Mkuu wa Bangladesh amesisitiza kuwa, ni jukumu la Umoja wa Mataifa kuwatengea eneo la amani wakimbizi wa jamii ya Rohingya ndani ya ardhi ya Myanmar, ili waweze kurejea nchini kwao kutoka katika kambi za muda wa wakimbizi zilizoko nchini Bangladesh.
Ombi la Bi Sheikh Hasina Wazed kwa Umoja wa Mataifa linaonesha namna hali ya Waislamu ilivyo mbaya nchini Myanmar kiasi kwamba Waziri Mkuu wa nchi jirani ya Bangladesh ambaye anayaona kwa karibu mateso ya Waislamu hao amelazimika kuuomba Umoja wa Mataifa kutenga na kusimamia eneo la angalau kuwapunguzia mateso Waislamu hao ndani ya ardhi ya Myanmar. Hata hivyo cha kusikitisha ni kwamba, hadi hivi sasa si Umoja wa Mataifa na wala si baraza lake la usalama, bali hakuna hata chombo kimoja cha kimataifa kilichochukua hatua za maana za kuwadhaminia usalama Waislamu hao madhlumu.
Wachambuzi wa mambo wanaliona ni zuri pendekezo hilo la Waziri Mkuu wa Bangladesh la kutengwa eneo ndani ya ardhi ya Myanmar kwa ajili ya kuwadhaminia usalama Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaoteketezwa kinyama katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo. Wachambuzi hao aidha wanasema, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuwadhaminia usalama raia hao wasio na ulinzi. Hivi sasa wimbi kubwa la Waislamu wa jamii ya Rohingya wanamiminika nchini Bangladesh katika mazingira magumu mno ili kukwepa ukatili na jinai wanazofanyiwa na mabudha wa Myanmar. Hata hivyo, kufika kwao Bangladesh hakuna maana ya kumalizika mateso yao, bali huwa ni kwamba wamesalimika tu na jinai za mabudha, Mazingira wanayokumbana nayo katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh ni magumu sana. Alaakullihaal, weledi wa mambo wanasema, ni jambo lililo mbali kwa serikali ya Myanmar kuuruhusu Umoja wa Mataifa kutenga eneo salama kwa ajili ya Waislamu hao.
Sisitizo jingine la Waziri Mkuu wa Bangladesh la kutaka Umoja wa Mataifa utume timu yake katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar kwenda kuwalinda Waislamu, nalo ni pendekezo zuri. Kiujumla ni kwamba Umoja wa Mataifa una njia nyingi za kuweza kuishinikiza serikali ya Myanmar ikomeshe mauaji ya kimbari wanayofanyiwa Waislamu wa nchi hiyo, lakini inaonekana nia ya kweli ya kufanya hivyo haipo. Umoja wa Mataifa unaweza pia kuishinikiza serikali ya Myanmar kuwarejesha nyumbani wakimbizi laki nne waliokimbilia Bangladesh, ingawa hilo nalo linaonekana ni jambo lililo mbali kwa Umoja wa Mataifa ambao umeonesha udhaifu mkubwa katika matukio mengi ya dunia. Ni jambo lililo mbali kwa Umoja wa Mataifa kufanya hivyo kwa sababu, hadi sasa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa dhidi ya serikali ya Myanmar. Si hayo tu, lakini pia kimya cha madola ya kibeberu na upuuzaji wa vyombo vyao vya habari ni idhini ya wazi kwa mabudha wa Myanmar kuendelea kufanya ukatili na uhayawani wao dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya bila ya kuogopa chochote.