UN: Waislamu wa Rohingya, mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34793-un_waislamu_wa_rohingya_mgogoro_mkubwa_zaidi_wa_wakimbizi_duniani
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa, kitendo cha wanajeshi na mabudha wa Myanmar cha kuwalazimizisha Waislamu wa Rohingya wakimbie makazi yao kimesababisha kuzuka mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 24, 2017 10:22 UTC
  • UN: Waislamu wa Rohingya, mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa, kitendo cha wanajeshi na mabudha wa Myanmar cha kuwalazimizisha Waislamu wa Rohingya wakimbie makazi yao kimesababisha kuzuka mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.

Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya wakimbizi amesema hayo leo Jumapili nchini Bangladesh ambayo ina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Myanmar na kuongeza kuwa, tangu tarehe 25 Agosti hadi hivi sasa, dunia inashuhudia idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wanaokimbia mauaji huko Myanmar na suala hilo limeufanya mgogoro wa wakimbizi hao kuwa mkubwa zaidi duniani.

Waislamu wa Myanmar, jamii inayodhulumiwa zaidi duniani

 

Amesema, wakimbizi hao wanateseka kwa kukosa chakula, maji, makazi na huduma za matibabu.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya wakimbizi ameongeza kuwa, Waislamu laki nne na 30 elfu wa jamii wa Rohingya waliolazimika kukimbilia Bangladesh katika kipindi cha mwezi mmoja tu kutokana na ukatili wanaofanyiwa nchini kwao, wanahitajia misaada mingi sana. Ameitaka jamii ya kimataifa kuongeza misaada yake kwa Bangladesh kadiri inavyowezekana kutokana na nchi hiyo kujitolea kuwapokea wakimbizi hao.

Wahanga wakuu wa ukatili wa mabudha na wanajeshi wa Myanmar ni wanawake na watoto wadogo wa Kiislamu

 

Kuanzia tarehe 25 Agosti hadi hivi sasa, mabudha na wanajeshi wa Myanmar wanafanya ukatili mkubwa sana dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya hasa wa mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa nchi hiyo. Zaidi ya Waislamu elfu sita wameshauwa na elfu nane wengine kujeruhiwa hadi hivi sasa kutokana na ukatili huo.