Kuanza mazungumzo baina ya Bangladesh na Myanmar kuhusu kurejea wakimbizi Warohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35191-kuanza_mazungumzo_baina_ya_bangladesh_na_myanmar_kuhusu_kurejea_wakimbizi_warohingya
Waziri Mkuu wa Bangladesh ametoa habari ya kuanza mazungumzo kati ya nchi yake na serikali ya Myanmar kwa ajili ya kuwarejesha makwao kwa akali wakimbizi nusu milioni ambao ni Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia katika nchi hiyo jirani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 04, 2017 02:20 UTC
  • Kuanza mazungumzo baina ya Bangladesh na Myanmar kuhusu kurejea wakimbizi Warohingya

Waziri Mkuu wa Bangladesh ametoa habari ya kuanza mazungumzo kati ya nchi yake na serikali ya Myanmar kwa ajili ya kuwarejesha makwao kwa akali wakimbizi nusu milioni ambao ni Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia katika nchi hiyo jirani.

Sheikh Hasina Wazed  sanjari na kuonyesha wasiwasi alionao kutokana na kuendelea jinai za serikali ya Myanmar na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu Warohingya katika jimbo la Rakhine amesema kuwa, serikali ya Dhaka iko tayari kufanya mazungumzo na serikali ya Myanmar kwa ajili ya kuwarejesha wakimbizi wa Kirohingya katika nchi yao.

Aidha Waziri Mkuu huyo ameutaka Umoja wa Mataifa utume timu ya kutafuta ukweli ili ikajionee kwa karibu hali wanayokabiliwa nayo Waislamu wasio na ulinzi wa Rohingya.

Ombi la Waziri Mkuu huyo wa Bangladesh linatolewa katika hali ambayo, hadi sasa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama hazijachukua hatua za maana na athirifu kwa ajili ya kukomesha mauaji ya kimbari katika jimbo la Rakhine huku serikali ya Myanmar ikiwazuia wawakilishi wa Umoja wa Mataifa kutembelea jimbo hilo linaloshuhudia mauaji dhidi ya Waislamu.

Sheikh Hasina, Waziri Mkuu wa Bangladesh

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu. 

Matamshi ya Sheikh Hasina, kuhusiana na kuanza mazungumzo na serikali ya Myanmar kwa ajili ya kurejea wakimbizi Waislamu Warohingya katika nchi yao yanatolewa katika hali ambayo, nchi hiyo jirani na Myanmar imeendelea kushuhudia wimbi la wakimbizi Waislamu. Kutokana na mazingira tofauti ya kisiasa, serikali ya Bangladesh imeamua kuchagua njia ya kufanya mazungumzo na serikali ya Myanmar kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa wakimbizi.

Serikali ya Bangladesh ambayo kuanzia mwezi Agosti hadi sasa imekuwa ikikabiliwa na wimbi la wakimbizi sambamba na kushadidi ukandamizaji na jinai za jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu Warohingya, katika wiki za hivi karibuni imetangaza mara kadhaa kwamba, mbali na kuwa haiwezi kudhamini peke yake mahitaji ya takribani wakimbizi laki tano wa Kirohingya imesisitiza kwamba, suala la kuwapatia makazi wakimbizi hao lilikuwa la muda tu na kwamba, jamii ya kimataifa inapaswa kuwashinikiza viongozi wa Myanmar ili waandae mazingira ya kurejea nyumbani wakimbizi hao wa Kiislamu.

Wakimbizi Waislamu wa Rohingya wakiwa nchini Bangladesh

Hata hivyo takwa la serikali ya Bangladesh kwa jamii ya kimataifa la kuwapatia misaada ya haraka wakimbizi wa Kiislamu wa Myanmar katika mipaka ya pamoja ya nchi hiyo na Myanmar na jamii ya kimataifa kuwashinikiza viongozi wa Myanmar ili waandae mazingira ya kurejea wakimbizi wa jamii ya Rohingya halijapewa umuhimu na asasi husika likiwemo Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, Umoja wa Mataifa na hata Baraza la Usalama.

Katika mazingira kama haya, serikali ya Bangladesh imeamua kutanguliza mbele siasa za mazungumzo na viongozi wa Myanmar ikiwa na matumaini kwamba, kupitia mazungumzo na katika fremu ya mpango wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi Waislamu wa Rohingya itaweza kuipatia ufumbuzi sehemu ya matatizo yanayosababishwa na mamia ya wakimbizi hao.

Pamoja na kuripotiwa kuanza mazungumzo baina ya Bangladesh na Myanmar kwa ajili ya kutafuta njia ya kuwarejesha makwao wakimbizi hao, lakini hadi sasa hakuna mazingira yoyote yaliyoandaliwa kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo.

Wanajeshi wa Myanmar wanaotuhumiwa kutenda jinai dhidi ya Waislamu katika jimbo la Rakhine

Hii ni kutokana na kuwa, jeshi la Myanmar likishirikiana na Mabudha wa nchi hjiyo wenye misimamo ya kufurutu ada wanaendelea na hujuma na jinai zao dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na hivyo kuwafanya watu wengine zaidi kuyakimbia makazi yao na kuelekea upande wa maeneo ya mpakani na Myanmar.

Hata kama katika siku za hivi karibuni kumeripotiwa habari ambayo haijathibitishwa kuhusiana na serikali ya Myanmar kukubali kurejea wakimbizi wa Rohingya, lakini kuna hofu kwamba, endapo watarejea watakabiliwa na hujuma na vitendo vya ukandamizaji zaidi na hivyo kuwafanya wakabiliwe na hali mbaya zaidi katika jimbo la Rakhine kuliko ilivyokuwa hapo kabla.