Afisa mkuu wa UN ajiuzulu kutokana na jinai za Israel
-
Makarim Wibisono
Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo, kutokana na kile alichokitaja kuwa ukosefu wa ushirikiano wa utawala wa kizayuni wa Israel.
Makarim Wibisono, ambaye alichukua wadhifa huo Juni mwaka 2014, amesema utawala haramu wa Israel umekuwa kizingiti katika kazi yake kwa kumzuia afike maeneo aliyotakiwa kufanya uchunguzi wa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Hatua hii inajiri siku chache baada ya ripota huyo maalumu wa UN kusema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni mkiukaji wa haki za binadamu. Makarim Wibisono aliyasema hayo Februari 12 mwaka huu katika ripoti yake ya mwisho aliyoikabidhi kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya Wapalestina na hivyo kukiuka haki za binadamu. Ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu huko Palestina aliutaka utawala ghasibu wa Israel kuwakamata na kuwapandisha kizimbani wale wote wanaohusika na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina. Wakati huo huo, uteuzi wa atakayerithi mikoba ya Wibisono umeahirishwa baada ya watu wawili waliokuwa wamependekezwa kuchukua nafasi yake kutuhumiwa na utawala haramu wa Israel kuwa wana misimamo na ajenda dhidi ya utawala huo ghasibu. Wawili hao ni Penny Green, Profesa wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Uingereza na Michael Lynk, Profesa wa Sheria raia wa Canada.