Mogherini: JCPOA ni ushindi kwa ulimwengu na kwa wananchi wa Iran
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kwa mara nyengine tena umuhimu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na ulazima wa kuyalinda na ameeleza kwamba: kwa makubaliano haya ya kimataifa, ulimwengu pamoja na wananchi wa Iran wamepata ushindi.
Akizungumza nchini Ujerumani hapo jana, Federica Mogherini amesema makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 ni ya ushindi wa pande zote mbili na kubainisha kuwa kwa mujibu wa ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi sasa imetekeleza ahadi zake zote kuhusiana na JCPOA.
Huku akiashiria kwamba JCPOA ni milki ya Jamii ya Kimataifa, Mkuu wa Sera za Nje wa EU amesema: haya si makubaliano yaliyoratibiwa baina ya nchi mbili na kuweza kuyafanyia mabadiliko.
Siku ya Ijumaa iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani, bila kujali ripoti nane za IAEA ambazo zimesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeheshimu na kutekeleza kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, alitangaza kuwa hatothibitisha kuwa Tehran imetekeleza makubaliano hayo.
Baada ya hatua hiyo ya Trump ambayo inalenga kuyavunja makubaliano hayo ya kimataifa, Kongresi ya Marekani itakuwa na muda wa siku 60 kupitisha uamuzi kuhusu kuiwekea tena Iran vikwazo, ambavyo utekelezaji wake utahitaji kusimamishwa utekelezaji wa JCPOA, na ikiwa itapiga kura ya kurejeshwa na kutekelezwa tena vikwazo hivyo, Marekani itajitoa kwenye makubaliano hayo.
Trump amekuwa kila mara akidai kuwa JCPOA ni makubaliano mabaya zaidi iliyowahi kusaini Marekani na kutaka yavunjwe; msimamo ambao umekosolewa vikali na Jamii ya Kimataifa wakiwemo washirika wengine wa Washington katika makubaliano hayo ambao ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Russia na China na hata viongozi wengi ndani ya Marekani kwenyewe.
Mara baada ya matamshi yaliyotolewa na Trump siku ya Ijumaa, Umoja wa Ulaya ulisisitiza kwa mara nyengine tena kuwa utaendelea kuunga mkono makubaliano hayo ya nyuklia.../