Oct 20, 2017 17:14 UTC
  • Makumi ya Waislamu wauawa msikitini mjini Kabul, Daesh yajigamba imehusika

Waislamu wasiopungua 32 wameuawa shahidi leo katika shambulizi la kigaidi lililofanyika ndani ya msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Shambulizi hilo la kigaidi limelenga Msikiti wa Imam Zaman wakati waumini walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Swala ya Magharibi.

Maafisa usalama wa Afghanistan wanasema idadi ya wahanga iliyotangazwa hadi sasa wa shambulizi hilo ni ya awali na kwamba kuna uwezekano idadi kamili ikaongezeka.

Kundi la kiwahabi na kigaidi la Daesh limejigamba kuwa ndilo lililofanya shambulizi hilo ndani ya Msikiti wa Imam Zaman.

Mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia yameongezeka sana nchini Afghanistan. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba magaidi waliokuwa na mabomu walijilipua ndani ya msikiti wa Waislamu wa madhehebu hiyo na kuua waumini 8. Mwezi Agosti pia magaidi wa kiwahabi walishambulia msikiti wa Shia mjini Kabul na kuua waumi wasiopungua 40.

Mawahabi wamezidisha mashambulizi dhidi ya misikiti ya Shia Afghanistan

Itakumbukwa kuwa mwaka 2011 pia mawahabi walishambulia shughuli ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika misikiti kadhaa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na kuua shahidi waumini zaidi ya 80 wakiwemo wanawake na watoto wadogo.

Tags