Mahakama ya Pakistan yaagiza kukamatwa Waziri Mkuu wa zamani
Mahakama moja nchini Pakistan imetoa waranti wa kukamatwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Nawaz Sharif, baada ya kukosa kufika mahakamani kusikiliza kesi ya ufisadi inayomwandama.
Kadhalika Jaji Mohammad Bashir wa makahama hiyo amepuuzilia mbali ombi la wakili wa Nawaz Sharif la kutaka mteja wake aruhusiwe kutofika mahakamani ili asalie mjini London anakomuuguza mkewe ambaye amelazwa hospitalini.
Kwa mujibu wa sheria za Pakistan, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo anaweza kukamatwa mara tu atakapowasili nchini humo akitokea nchini Uingereza na iwapo hatakuwa amepewa dhamana na koti kabla ya kikao kijao cha kesi dhidi yake. Jaji huyo amesema kesi hiyo itasikilizwa tena Novemba 3.
Oktoba 19, mahakama ya Pakistan ilisikiliza rasmi kesi ya mashtaka ya ufisadi inayomkabili Muhammad Nawaz Sharif na familia yake, ambayo inaweza kupelekea kiongozi huyo kuhukumiwa kifungo jela.
Mashtaka ya ufisadi yanayomkabili Nawaz Sharif na watu wanne wa familia yake wakiwemo watoto wake yanatokana na uchunguzi uliofanywa kupitia nyaraka zilizotolewa na kampuni ya kisheria ya Panama iliyofichua kuwa Sharif anamiliki mali ambazo hajazitangaza nje ya nchi.
Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Pakistan mwenye umri wa miaka 67, alilazimika kuachia ngazi mwezi Julai mwaka huu, baada ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kumuengeu madarakani kutokana na kesi za rushwa zinazomuandama.