Seneta McCain: Iran itaitimua Marekani Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35962-seneta_mccain_iran_itaitimua_marekani_mashariki_ya_kati
John McCain, Mkuu wa Kamati ya Vikosi vya Ulinzi ya Seneti ya Marekani ameiasa serikali ya Washington iwe na stratijia inayofahamika ya kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinginevyo, Iran itaitimua Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2025-12-03T16:38:35+00:00 )
Oct 26, 2017 15:11 UTC
  • Seneta McCain: Iran itaitimua Marekani Mashariki ya Kati

John McCain, Mkuu wa Kamati ya Vikosi vya Ulinzi ya Seneti ya Marekani ameiasa serikali ya Washington iwe na stratijia inayofahamika ya kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinginevyo, Iran itaitimua Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Gazeti la New York Times la Marekani limemnukuu McCain ambaye pia ni seneta mwandamizi wa chama cha Republican  akisema kuwa, hivi sasa Washington inakabiliwa na hatari kubwa kutokana na kile alichokidai kuwa ni kukosekana kwa stratijia iliyokamilika kuhusiana na eneo la Mashariki ya Kati na utata wa eneo hilo. Akitaja mafanikio ya kieneo iliyopata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi za Iraq, Syria na Yemen McCain amedai kuwa, Tehran inaendelea kuyafanyia majaribio makombora yake ya balestiki huku nchi za Kiarabu waitifaki wa Marekani zikivutana na Qatar licha ya kuwepo kitisho muhimu zaidi kwao alichodai kuwa ni Iran. 

Wasi wasi wa Marekani wa kutimuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutoka nchi za Kiislamu

McCain ametahadharisha kwamba Washington inatakiwa kuyapa umuhimu yanayojiri katika eneo la Mashariki ya Kati, kwani itafikia wakati ushawishi wa Marekani katika eneo hilo lenye umuhimu duniani utatoweka. Inafaa kuashiria kuwa, sambamba na kusambaratika kwa makundi ya kigaidi na ukufurishaji hususan Daesh (ISIS), Jab'hatu Nusra na mfano wa hayo huko Iraq na Syria kulikotokana na juhudi za majeshi ya nchi hizo kwa kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, maafisa mbalimbali wa Marekani wamekuwa wakizidi kutoa kauli kali za kushambulia na kukosoa siasa za Washington katika Mashariki ya Kati.