Abdullah Abdullah: Askari wa kigeni waondoke nchini Afghanistan, hatuwahitaji
Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan, Abdullah Abdullah amewataka askari wa kigeni wanaoongozwa na Marekani waondoke nchini humo.
Abdullah Abdullah ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha Afghanistan ambapo pamoja na mambo mengine amewataka askari hao wa kigeni kuanza kuondoka nchi hiyo akibainisha kwamba raia wa Afghanistan wanapinga uwepo wa askari wa kigeni nchini mwao.
Kadhalika amesema kuwa, viongozi wa serikali ya Kabul wanatakiwa kufanya juhudi kubwa ili kujitosheleza na kutokuwa na mahitaji ya misaada ya askari wa kigeni ndani ya nchi yao. Wakati huo huo, Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan ameitaka jamii ya kimataifa kuheshimu ahadi zake kuhusiana na kadhia ya Afghanistan. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Afghanistan kuwataka askari wa kigeni wanaoongozwa na Marekani kuondoka nchini humo.
Kuondoka askari wa kigeni nchini humo ni moja ya masharti muhimu ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Taleban kwa ajili ya kupatana na serikali ya Kabul ambapo kwa mara kadhaa kundi hilo limekuwa likisisitizia suala hilo. Hadi sasa karibu askari elfu 14 wa kigeni wakiwemo askari elfu 11 kutoka Marekani, wapo nchini Afghanistan. Waafghani wanaamini kuwa, uwepo wa askari wa kigeni ndani ya taifa lao ndio chanzo cha ukosefu wa amani na kuendelea kuongezeka makundi ya kigaidi kama vile Daesh na Taleban sambamba na kuongezeka pia uzalishaji wa madawa ya kulenya.