Guterres: Umoja wa Mataifa umeazimia kulinda mazingira
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuhusu azma ya umoja huo ya kulinda mazingira duniani.
Antonio Guterres amesema kuwa Umoja wa Mataifa umeazimia kulinda mazingira kama nguzo kuu ya amani, usalama na ustawi endelevu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema hayo katika ujumbe alioutoa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Matumizi Mabaya ya Mazingira Vitani na Katika Mizozo ya Silaha iliyoadhimishwa leo Novemba 6.
Guterres amesema kuwa maafa yanayosababishwa kwa mazingira ni janga linaloweza kuendelea kwa miongo na miongo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kutiwa wasiwasi na taathira za mapigano na kuongeza kuwa vita vimekuwa na maafa makubwa kwa shughuli za viwanda na mazingira. Antonio Guterres aidha amewatolea mwito walimwengu kufanya juhudi ili kupunguza maafa yanayosababishwa na vita na mizozo ya silaha na kulinda maliasili zinazohitajika kwa ajili ya ustawi endelevu.