Askari wa US 'wapewa kibali' cha kuwabaka watoto wadogo nchini Afghanistan
Wanajeshi wa Marekani waliotumwa nchini Afghnistan walifahamishwa kuwa suala la vijana kubakwa hususan wa kiume wa nchi hiyo ni utamaduni unaokubalika.
Ripoti mpya ya kurasa 106 imefichua kuwa, Kamandi ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) nchini Afghanistan imekataa kushughulikia kesi za vijana kubakwa, ikisema kuwa uozo huo ni utamaduni unaokubalika katika jamii za nchi hiyo ya Asia.
Ripoti hiyo imedai kuwa, wanajeshi na maafisa usalama wa Afghanistan (ANDSF) wamekuwa wakiwalawiti vijana wadogo kila uchao.
Rais Donald Trump wa Marekani ambaye katika kampeni zake za kugombea urais aliahidi kuviondoa vikosi vya nchi hiyo nchini Afghanistan, mwezi Agosti mwaka huu alighairi msimamo huo na kusema kuwa wanajeshi hao watasalia nchini humo kwa muda usiojulikana.
Mapema mwezi huu, Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan, Abdullah Abdullah aliwataka askari wa kigeni wanaoongozwa na Marekani waondoke nchini humo, akisisitiza kwamba raia wa Afghanistan wanapinga uwepo wa askari wa kigeni nchini mwao.
Hadi sasa karibu askari elfu 14 wa kigeni wakiwemo elfu 11 kutoka Marekani, wapo nchini Afghanistan.