ICC kuchunguza jinai za Marekani nchini Afghansitan
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imeanza kufanya uchunguzi kuhusu jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizotekelezwa na majeshi yanayoongozwa na Marekani nchini Afghanistan.
Katika taarifa Jumatatu, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Fatou Bensouda amesema atachunguza jinai ambazo zimetekelezwa Afghanistan tokea Mei 1, 2003. Marekani ilianzisha hujuma ya kijeshi dhidi ya Afghanistan mwaka 2001 kwa madai kuwa kundi la Taliban ambalo lilikuwa linaongoza nchi hiyo lilikuwa limempa hifadhi kinara wa kundi la al-Qaeda aliyeuawa, Osama Bin Laden, ambaye alidai kuhusika na hujuma za kigaidi za Septemba 11, mwaka 2001 nchini Marekani.
ICC imesema itachunguza jinai za kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu uliotekelezwa na Marekani na waitifaki wake huku shirika kuu la ujasusi la nchi hiyo CIA likiangaziwa zaidi kutokana na kumiliki magereza ya siri huko Afghanistan na maeneo mengine duniani.
ICC imesema pia itachunguza jinai ambazo zinawezakuwa zimetekelezwa na kundi la Taliban na Jeshi la Afghanistan.
Mahakama hiyo ya ICC inachukua hatua hiyo baada ya kulaumiwa vikali kwa kutofuatilia kesi za jinai za madola makubwa duniani.