Kukiri shirika la Kimarekani kuwa limekwenda Afghanistan kupora madini
Kwa mara ya kwanza kabisa, shirika la Kimarekani-Kizayuni la Blackwater limekiri kuwa madini ndiyo yaliyolivutia kwenda nchini Afghanistan.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Erik Prince anasubiri vita vya Afghanistan viendelee na visiwe na mshindi ili atumie fursa hiyo ya watu kushughulishwa na vita, kuchimba madini ambayo ni nadra kupatikana duniani na ambayo yana thamani inayopindukia dola bilioni 3 za Kimarekani.
Hii ni mara ya kwanza kwa shirika hilo la Kimarekani-Kizayuni kukiri waziwazi kuwa limetuma vikosi vyake vya mauaji huko Afghanistan kwa ajili ya kupora utajiri mkubwa wa madini wa nchi hiyo ya Waislamu. Inatathminiwa kuwa Afghanistan ina utajiri wa madini wa dola trilioni moja na inaonekana lengo hasa la kutumwa wanajeshi wa Marekani nchini humo ni kupora utajiri huo mkubwa sana.
Katika miaka ya mwanzoni mwa urais wa Rais Hamid Karzai wa Afghanistan shirika hilo la Kimarekani-Kizayuni la kulinda usalama lilituhumiwa kuwa na jela za siri ndani ya ardhi ya Afghanistan.
Shirika hilo la Blackwater lina faili jeusi la kutenda jinai katika nchi za Iraq na Afghanistan kwa madai ya kutoa huduma za kiusalama. Miongoni mwa jinai zilizofanywa na shirika hilo la Kimarekani-Kizayuni ni mauaji ya kutisha dhidi ya raia wa nchi hizo mbili ambayo hatimaye yalipelekea shirika hilo kufukuzwa katika nchi hizo kutokana na mashinikizo makubwa ya wananchi wa Iraq na Afghanistan.
Mkurugenzi na muasisi wa shirika hilo la Blackwater amezusha suala la kulinda utajiri wa madini nchini Afghanistan katika hali ambayo shirika hilo lina jina baya sana nchini humo. Hivi sasa linadai kuwa liko tayari kulinda usalama wa migodi ya madini hayo ili lipate fursa nzuri ya kupora utajiri wa nchi hiyo.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa shirika la Blackwater ambalo linatumia fursa ya mgogoro wa Afghanistan kujinufaisha kiuchumi kadiri inavyowezekana, linaihesabu sekta ya madini ya nchi hiyo ya Waislamu kuwa ni fursa nzuri kwake ya kufikia malengo yake haramu.
Takwimu zilizotolewa zinaonesha kuwa, Afghanistan ina utajiri wa madini wenye thamani ya dola bilioni elfu tatu za Kimarekani, ingawa baadhi ya wataalamu wanasema kuwa, takwimu hizo ni chache ikilinganishwa na utajiri hasa wa madini ya nchi hiyo ya Waislamu.
Mwaka 2010 Wahidullah Shahrani, waziri wa wakati huo wa madini wa Afghanistan aliwaambia wandishi wa habari kuwa, hadi wakati huo kulikuwa kuna maeneo 28 yenye utajiri mkubwa wa madini yaliyogunduliwa nchini humo na inatathminiwa kuwa madini hayo yana thamani ya dola trilioni tatu za Kimarekani.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, zaidi ya asilimia 70 ya ardhi ya Afghanistan ilikuwa haijafanyiwa uchunguzi wa kugundua maeneo yenye madini na inatabiriwa kuwa, utajiri wa maliasili wa nchi hiyo yakiwemo madini una thamani kubwa mno inayopindukia kwa mbali takwimu zilizotolewa mwaka 2010.
Hivi sasa shirika la Kimarekani-Kizayuni la Blackwater limezuka na mpango wa kushiriki kulinda maeneo ya madini nchini Afghanistan katika hali ambayo, pendekezo la shirika hilo la kushiriki katika vita vya nchi hiyo mwezi Agosti mwaka huu halikupata uungaji mkono lilioutarajia. Shirika hilo lilitaka askari wake wachukue nafasi za wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan, lakini pendekezo hilo lilipingwa ndani ya Afghanistan bali hata ndani ya Marekani kwenyewe.
Wapinzani wa mpango huo wa Blackwater wamesema kuwa pendekezo hilo ni la kipuuzi na ni la hatari sana ambalo linaweza kuvipeleka vita vya Afghanistan katika upande usiotabirika kabisa.
Mtazamo mwingine wenye nguvu nchini Afghanistan ni kwamba, uamuzi wa shirika la Kimarekani-Kizayuni la Blackwater wa kuingilia kwa pupa suala la Afghanistan si tishio kwa usalama tu, bali hatua yake hiyo inaonesha ni kiasi gani shirika hilo lina uchu wa kupora vibaya utajiri wa wananchi wa Afghanistan kwa njia yoyote ile hata ya kutoa mapendekezo yasiyoingilika akilini.