Pakistan yaikosoa Marekani kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37989-pakistan_yaikosoa_marekani_kwa_kutoa_tuhuma_zisizo_na_msingi_dhidi_yake
Msemaji wa jeshi la Pakistan amejibu matamshi yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Marekani akiwa huko Afghanistan, kuwa mtazamo wa Washington dhidi ya Islamabad ni kikwazo katika mchakato wa mapambano dhidi ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2017 23:54 UTC
  • Pakistan yaikosoa Marekani kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi yake

Msemaji wa jeshi la Pakistan amejibu matamshi yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Marekani akiwa huko Afghanistan, kuwa mtazamo wa Washington dhidi ya Islamabad ni kikwazo katika mchakato wa mapambano dhidi ya ugaidi.

Akijibu matamshi hayo ya Mike Pence Makamu wa Rais wa Marekani, Meja Jenerali Asif Ghafoor ameeleza kuwa wanajeshi wa Pakistan wamechukua hatua zinazohitajika dhidi ya magaidi na kwamba hadi sasa hakuna nchi yoyote iliyochukua hatua kama za Pakistan katika kupambana na ugaidi. Mike Pence hivi karibuni alifanya safari huko Afghanistan ambapo alikariri vitisho vya Marekani dhidi ya Pakistan na kutangaza kuwa White House imeitaarifu Pakistan kuwa nchi hiyo itapoteza vitu vingi iwapo itaendelea kuyaunga mkono makundi ya kigaidi.

Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani  

Hali ya mvutano katika uhusiano wa Pakistan na Marekani ilianza tangu mwaka 2006 mwishoni mwa duru ya urais wa George W. Bush. Hata kama George Bush aliishukuru Pakistan kwa ushirikiano wake katika uvamizi wa Marekani huko Afghanistan mwaka 2001 na kuitaja nchi hiyo kuwa muitifaki wa Marekani ambaye si mwanachama wa Muungano wa Nato, lakini kuzama kwenye kinamasi wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan, kumewapelekea viongozi wa kijeshi na kisiasa wa nchi hiyo kuituhumu serikali ya Pakistan kuwa haijashirikiana  kwa dhati na jeshi la Marekani huko Afghanistan.

George W.Bush, Rais mstaafu wa Marekani  

Hali ya mvutano katika uhusiano wa nchi mbili hizo iliongezeka mara baada ya kuanza mashambulizi ya anga ya Marekani katika maeneo ya kikabila nchini  Pakistan; huku tuhuma zinazotolewa na viongozi wengine wa Marekani dhidi ya Pakistan zikiongezeka maradufu  baada ya kuingia madarakani huko White House Rais Donald Trump; hali iliyoathiri  mlingano na ushirikiano wa kieneo wa nchi hizo.  

Mahmoud Shah Afsar Mtaalamu wa masuala ya Kijeshi nchini Pakistan anasema: Marekani haina lengo la kurejesha amani  huko Afghanistan; bali inafanya kila iwezalo ili kuzuia maendeleo ya kiuchumi ya baadhi ya nchi kwa kuvuruga mchakato wa amani na kuituhumu Pakistan; na ndio maana Washington inaiunga mkono na kuikingia kifua India.  

Katika hotuba zake mbalimbali, Rais Donald Trump wa Marekani ameituhumu Pakistan kuwa inaunga mkono ugaidi; na hivi karibuni pia akitangaza stratejia ya Marekani huko Afghanistan na vile vile stratejia mpya ya usalama wa taifa la Marekani, Rais Donald Trump kwa mara nyingine tena alitangaza wazi kuwa Pakistan ni mahali salama kwa makundi ya kigaidi; matamshi yaliyokabiliwa na radiamali ya Islamabad. Marekani inatumia wenzo wa kuishinikiza Pakistan kupitia njia ya kuipunguzia misaada ya kifedha na kijeshi; misaada ambayo imekuwa ikiitumia kama wenzo wa kuishawishi Islamabad ishirikiane nayo. Hata hivyo, je, siasa za utumiaji mabavu na za vitisho za Marekani dhidi ya Pakistan kuhusu  Afghanistan zitakuwa na jibu la kuridhishwa kwa Washington au la? Weledi wa mambo wa Marekani wanatoa jibu hasi kwa jambo hilo kwa sababu kwa hali yoyote ile nchi hiyo inaihitajia Pakistan ili kufanikiwa huko Afghanistan. 

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Marekani Bi Elizabeth Warren anasema: Serikali ya Trump inapuuza nafasi ya mazungumzo ya amani huko Afghanistan ili kuhitimisha vita nchini humo". Mashinikizo ya kati na kati yanahitajika kwa serikali ya Pakistan ili kusaidia mchakato huu; hii ni kwa sababu hatuwezi kutumia njia za kijeshi pekee kuwashawishi wapinzani wa serikali ya Afghanistan kufanya mazungumzo.