Uhispania yaendelea kuiuzia silaha Saudi Arabia, zinatumika kuua raia wa Yemen
Ripoti za Wizara ya Biashara ya Uhispania inaonesha kuwa, katika kipindi cha miezi sita ya mwanzoni mwaka huu wa 2017 serikali ya nchi hiyo imeidhinisha mauzo ya silaha na mizinga yenye thamani ya zaidi ya Euro milioni 141 kwa utawala wa Saudi Arabia.
Kwa msingi huo mashirika ya kutetea haki za binadamu kama Amnesty International yanaitaka Uhispania isimamishe uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia ambayo tangu ilipoanzisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen imenunua silaha zenye thamani ya Euro milioni 728 kutoka Uhispania.
Nchi za Ulaya zinaendelea kuiuzia Saudi Arabia silaha zinazotumiwa kushambulia na kuua watu wa Yemen kwa kuzingatia kile kinachotajwa kuwa ni maslahi yao makuu na ya nchi waitifaki wao licha ya suala hilo kukiuka sheria na kanuni zilizowekwa na nchi hizo zenyewe. Itakumbukwa kuwa tarehe 30 Novemba mwaka huu wa 2017 Bunge la Ulaya lilipasisha sheria iliyopiga marufuku uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia kutokana na ukiukaji wake mkubwa wa haki za binadamu nchini Yemen.
Baadhi ya nchi za Ulaya zinadai kuwa, silaha zinazouzwa na nchi hizo kwa utawala wa Saudi Arabia hazitumiki katika vita vya Yemen. Kwa mfano tu Marisa Ponsela ambaye ni Naibu Waziri wa Bishara wa Uhispania alidai mwezi uliopita wa Novemba kwamba: "Saudia na Imarati zinazoshiriki katika vita vya Yemen zimeahidi kuwa silaha zinazonunua kutoka Uhispania ni kwa ajili ya matumizi ya ndani." Hata hivyo ushahidi unaonesha kuwa silaha hizo zinatumiwa kuua raia wasio na hatia wa Yemen.
Nchi kubwa za Ulaya kama Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Uhispania ni miongoni mwa wauzaji wakuu wa silaha na zana za kivita kwa Saudi Arabia na zinachuma mabilioni ya Euro kutokana na mauzo hayo. Muungano wa vyama vya kijani katika Bunge la Ulaya siku chache zilizopita ulitoa wito wa kukomeshwa uuzali wa silaha kwa Saudi Arabia kutokana na ukiukaji wake mkubwa wa haki za binadamu na mauaji ya raia wasio na hatia huko Yemen na kusema: Masharti yaliyowekwa kwa ajili ya biashara hiyo yanakiukwa waziwazi. Si hayo tu bali nchi hizo za Ulaya katika miaka ya hivi karibuni si tu kwamba hazikusitisha uuzaji wa silaha kwa utawala wa Saudi Arabia unaoendelea kuua watoto wa Yemen, bali pia zimezidisha kiwango cha silaha zinazouzwa kwa utawala huo licha ya malalamiko ya walimwengu hususan jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu.
Sergey Syberibov ambaye ni mchambuzi wa siasa wa Russia anasema Marekani na Uingereza zinafaidika sana na vita na mashambulizi ya Saudi Arabia huko Yemen. Ameongeza kuwa nchi za Ulaya zinafumbia macho jinai na uhalifu mkubwa unaofanywa na utawala wa Saudia huko Yemen kwa kipindi cha miezi 33 sasa kwa shabaha ya na kuziunga mkono tawala tegemezi kwa Magharibi, kupata faida na kwa ajili ya kudumisha uhai wa makampuni yao ya kutengeneza silaha. Suala hili kwa upande mwingine linaonesha sura ya kindumakuwili na kinafiki ya nchi za Magharibi madai ya kutetea haki za binadamu.