Dec 30, 2017 04:27 UTC
  • Russia: Tupo tayari kuzipatanisha Marekani na Korea Kaskazini

Balozi wa Russia nchini Korea Kaskazini ametangaza utayarifu wa nchi yake wa kuwa mwenyeji wa mazungumzo tarajiwa kati ya Marekani na Korea Kaskazini.

Oleg Burmistrov amesema kuwa, wakati wowote kutakapotolewa ombi hilo kwa serikali ya nchi yake, Moscow itakuwa tayari katika uwanja huo. Burmistrov ameongeza kwa kusema kwamba, Russia imejiandaa kupokea simu kwa ajili ya kuandaa mahala kutakapofanyikia mazungumzo hayo.

Oleg A. Golubchikov

Katika siku za hivi karibuni, Dmitry Peskov, Msemaji wa ikulu ya Kremlin alitangaza kwamba, Russia iko tayari kuzipatanisha Marekani na Korea Kaskazini endapo Pyongyang na Washington zitataka kufanya mazungumzo baina yao.

Kabla ya hapo pia Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alizitaka Washington na Pyongyang kufanya mazungumzo kwa ajili ya kutatua mgogoro unaoendelea kuongezeka kila uchao kati ya nchi mbili. Hata hivyo wakati wanadiplomasia wa Marekani wakiendelea kufuatilia njia za udiplomasia kwa ajili ya kutatua mgogoro unaoendelea kati ya nchi mbili, Rais Donald Trump wa nchi hiyo ametangaza kwamba, kabla ya kuanza kwa mazungumzo yoyote Korea Kaskazini inatakiwa kwanza kuachana na silaha zake za nyuklia. 

Rais Donald Trump wa Marekani

Wakati huo huo, mhadhiri mmoja wa Korea Kusini amesema kuwa, Marekani haina uwezo wa kuzuia maendeleo ya makombora ya balestiki na silaha za nyuklia ya Korea Kaskazini. Andre lencyf mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kookmin nchini Korea Kusini amesema kuwa Washington imeshindwa kuzuia maendeleo ya silaha za Korea Kaskazini. Ameongeza kwamba Pyongyang inataka kuzalisha makombora ambayo yataweza kuishambulia Marekani wakati kutakapotokea vita na kwamba tayari Korea Kaskazini imepata uwezo huo.

Tags