EU kufanya mkutano wa dharura wa wafadhili wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38809-eu_kufanya_mkutano_wa_dharura_wa_wafadhili_wa_palestina
Umoja wa Ulaya na Norway zinatazamiwa kufanya kikao cha dharura cha nchi wafadhili wa Palestina karibuni hivi, baada ya Marekani kutishia kuikatia misaada taasisi ya Umoja wa Mataifa inayoshuughulikia wakimbizi wa Kipalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2018 04:21 UTC
  • EU kufanya mkutano wa dharura wa wafadhili wa Palestina

Umoja wa Ulaya na Norway zinatazamiwa kufanya kikao cha dharura cha nchi wafadhili wa Palestina karibuni hivi, baada ya Marekani kutishia kuikatia misaada taasisi ya Umoja wa Mataifa inayoshuughulikia wakimbizi wa Kipalestina.

Taarifa ya EU imesema mkutano huo usio wa kawaida utafanyika Januari 31 mjini Brussels chini ya uenyekiti wa Norway.

Mapema mwezi huu, Rais Donald Trump wa Marekani alitishia kwamba atakata misaada ya kifedha kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa kutoonyesha nia ya kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Januari 2, Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: 'Wapalestina hawataki mazungumzo ya amani, kwa nini tuendelee kuwapa misaada? Tunawapa Wapalestina mamia ya mamilioni ya dola kila mwaka na wala hawaonyeshi shukrani wala heshima.'

Mwaka jana Trump alilaaniwa kote duniani kwa tangazo lake dhidi ya Quds Tukufu

Hapo jana shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch liliikosoa vikali serikali ya Washington kwa kutishia kuwakatia misaada wakimbizi wa Kipalestina, na kutaja hatua hiyo kama usaliti.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema hatua ya Marekani ya kukata msaada wa fedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) na pia kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina endapo haitokuwa tayari kufanya mazungumzo na mapatano na adui Mzayuni ni ghilba ya kisiasa.