Ujerumani yaacha kuiuzia silaha Saudia na wavamizi wa Yemen
Serikali ya Ujerumani imesitisha kuiuzia silaha Saudia na karibu waitifaki wenzake wote wanaoshiriki katika jinai dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Yemen.
Hatua hiyo ya Ujerumani inatabiriwa kuusababishia matatizo utawala wa ukoo wa Aal Saud na wavamizi wenzake wa Yemen ambao wanatumia silaha za nchi za Magharibi kufanya jinai za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa Yemen.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert amesema kuwa, Baraza la Usalama la Shirikisho la Ujerumani halitatoa tena kibali cha kuuza silaha kwa nchi zisizoheshimu mikataba na masharti ya kuuziwa silaha.
Uamuzi huo umechukuliwa katika mazungumzo baina ya vyama vya kisiasa vya Ujerumaini vya Christian Democratic Union, Christian Social Union na Social Democrats kuhusiana na kuunda serikali mpya ya pamoja nchini Ujerumani.
Muswada wa makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo kuhusiana na uuzaji wa silaha nje ya Ujerumani unasema: "serikali ya shirikisho itaacha mara moja kuziuzia silaha nchi zinazohusika na vita vya Yemen."
Hadi sasa watu 13,600 wameripotiwa kuuawa tangu Saudi Arabia ilipoanzisha vita vya kivamizi dhidi ya nchi ya Kiarabu ya Yemen mwezi Machi 2015. Kundi hilo linalofanya jinai nchini Yemen linaundwa na Saudia, Imarati, Jordan, Misri, Bahrain, Kuwait, Morocco, Sudan na Senegal kwa msaada wa silaha kutoka nchi za Magharibi hususan Marekani na Uingereza.
Itakumbukwa kuwa, mwaka jana Marekani ilitiliana saini na Saudi Arabia mkataba wa silaha wa dola bilioni 110; silaha ambazo sehemu yake kubwa zinatumika kuulia Waislamu kwa mikono ya tawala vibaraka za nchi za Waislamu wenyewe.
Nchi zinazofanya jinai nchini Yemen zina wasiwasi kwamba huenda nchi nyingine za Magharibi nao zikafuata mkondo wa hatua ya Ujerumani ya kuacha kuziuzia silaha nchi hizo, na hivyo kutoa pigo kubwa kwao.