Radiamali ya Russia kwa tuhuma za Waziri wa Ulinzi wa Uingereza
Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa, tuhuma zilizotolewa na Waziri wa Ulinzi wa Uingereza dhidi ya Russia ni za uongo.
Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Meja Jenerali Igor Konashenkov kuwa matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Gavin Williamson aliyadai kuwa Russia ina mpango wa kushambulia miundombinu na raia wa Uingereza yanatokana na njozi za waziri huyo.
Akizungumza katika mahojiano yake na gazeti la Daily Telegraph, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza alidai kuwa, Russia imeazimia kusababisha madhara kwa uchumi wa Uingereza na kuwauwa maelfu ya raia wa nchi hiyo.
Katika mahojiano hayo, Gavin Williamson aliongeza kuwa, Russia haina lengo la kuivamia kijeshi na kutuma wanajeshi wake nchini Uingereza, lakini inataka kuishambulia miundombinu ya nchi hiyo. Meja Jenerali Igov Konashenkov ambaye ni Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia amejibu madai hayo akisema kuwa Waziri wa Ulinzi wa Uingereza amekuwa njozini kwa muda mrefu katika jitihada za kutafuta vyanzo vya kifedha na kupata bajeti ya jeshi.
Uhusiano wa Russia na Uingereza katika miezi ya hivi karibuni umekumbwa na mivutano mingi na London inaituhumu Moscow kuwa inaingilia masuala ya uchaguzi ya nchi hiyo na katika nchi nyingine za Ulaya. Moscow imekanusha madai hayo na kusema hayana msingi.