Jan 30, 2018 08:01 UTC
  • WHO yaonya kuwa usugu wa viuavijasumu (antibiotics) ni tishio duniani

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani WHO kuhusu usugu wa viuavijasumu au antibiotics zinaonyesha kuwa juu sana kiwango cha usugu wa dawa hizo dhidi ya maradhi kadhaa yanayosababishwa na bakteria kote duniani.

Kwa mujibu wa mfumo mpya wa WHO wa ufuatiliaji wa kupambana na vijiumbe maradhi au antimicrobial unaojulikana kama (GLASS), takwimu hizo zimekusanywa miongoni mwa watu 500,000 walioathirika na vimelea na kutumia dawa kutoka nchi 22.

Ripoti ya WHO inasema kuna takribani vimelea saba ambavyo ni sugu dhidi ya dawa za viuavijasumu vikiwemo Staphylococcus(STAFILOKOKAS) , E.coli (IKOLAI) na salmonella (SALIMONELA) ingawa ripoti hiyo haijajumuisha takwimu za vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa kifua kikuu.

Wagonjwa katika Hospitali ya Kenyatta mjini Nairobi

WHO inasema takwimu hizo zinathibitisha kuwepo tatizo kubwa kote duniani. Hadi sasa kuna nchi 52 zilizoathirika na tatizo hili , 25 za kipato cha juu, 20 za kipato cha wastani na 7 za kipato cha chini ambazo zimeorodheshwa katika mfumo wa GLASS wa WHO.

WHO imeongeza kuwa ripoti hii ni hatua ya kwanza muhimu kuelekea kuboresha uelewa kuhusu kiwango cha usugu wa viuavijasumu na kisha kuchukua hatua madhubuti dhidi ya tishio hilo kubwa la kimataifa.

Tags