Feb 02, 2018 08:00 UTC
  • Homa ya mafua imeshaua watu 231 nchini Uingereza

Gazeti la Daily Mail linalochapishwa nchini Uingereza limeripoti kuwa watu 231 wamefariki dunia nchini humo kutokana na maambukizi ya kirusi cha homa ya mafua.

Likizinukuu duru rasmi za serikali, gazeti hilo limeandika kuwa watu 193 wamefariki dunia huko England, 26 Scotland na wengine 12 huko Ireland ya Kaskazini. Hakuna taarifa halisi za idadi ya vifo katika eneo la Wales.

Kwa mujibu wa ripoti ya Daily Mail, tangu ulipoanza msimu wa baridi unaoendelea hivi sasa, maelfu ya watu wamelazwa kwenye hospitali nchini Uingereza kutokana na maambukizi ya kirusi cha homa ya mafua huku idadi ya wagonjwa walioripoti kwenye vituo vya tiba kuwa na ishara za homa hiyo ikiongezeka mno.

Hali hiyo imesababisha kuongezeka matumizi ya chanjo ya homa ya mafua nchini Uingereza na kuwa adimu kupatikana katika siku za karibuni.

Chanjo ya homa ya mafua

Richard Pebody, mkuu wa kitengo cha maradhi ya upumuaji katika Shirika la Taifa la Huduma za Afya la Uingereza (National Health Service) amesema: tangu ulipoanza msimu wa baridi watu zaidi ya milioni moja na laki tano, ambayo ni idadi kubwa zaidi kulinganisha na miaka iliyopita, wamedungwa chanjo ya homa ya mafua.

Na hii ni katika hali ambayo, duru za nchini Uingereza zinaripoti kuwa wagonjwa wamekuwa wakifurika kwenye vitengo vya huduma za dharura vya hospitali huku kukiwepo na uhaba wa wafanyakazi wa kushughulikia tatizo hilo.

Ripoti ya karibuni kabisa kuhusu utendaji wa Shirika la Taifa la Huduma za Afya la Uingereza inaonyesha kuwa kwa uchache wagonjwa laki moja wamelazimika kusubiri kwa saa kadhaa ndani ya magari ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya kuhamishiwa kwenye vitengo vya huduma za dharura vya hospitali za nchi hiyo.../

Tags