Malengo ya safari ya Tillerson katika nchi za Amerika ya Latini
Rex Tillerson Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amedai akiwa Mexico katika safari yake ya kiduru ya kuzitembelea nchi za Amerika ya Latini kuwa Russia ina mpango wa kuingilia masuala ya uchaguzi ya nchi hiyo.
Akiwa jimboni Texas Marekani na kabla ya kuanza safari yake ya kuzitembelea nchi za Mexico, Argentina, Peru, Colombia na Jamaica, Tillerson aidha amezitahadharisha nchi hizo za Amerika ya Latini kuhusu kuimarisha ushirikiano wao na China na kudai kuwa eneo hilo halihitaji kuwa na mkoloni mpya. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ameanza safari yake hiyo ya kiduru huko Amerika ya Latini kwa kuzidhihirisha Russia na China kuwa tishio ili kwa upande mmoja aweze kufunika matatizo mengi yaliyopo baina ya Washington na nchi hizo za Amerika ya Latini na katika upande wa pili azuie kuimarishwa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya eneo hilo na nchi za Russia na China, eneo ambalo wakati mmoja lilikuwa chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa Marekani.
Hali ya mvutano katika uhusiano wa Marekani na nchi za Amerika ya Latini imeongezeka tangu Rais Donald Trump ashike hatamu za uongozi mwezi Januari mwaka jana. Trump amesitisha mchakato wa kuboresha mahusiano baina ya Washington na Havana na kutishia kuwa ataitoza serikali ya Mexico gharama kubwa ya kujenga ukuta wa mpakani kati ya Marekani na nchi hiyo. Serikali ya sasa ya Marekani pia imekusudia kuwarejesha katika nchi zao huko Amerika ya Latini mamia ya maelfu ya wahajiri haramu. Baadhi ya nchi za eneo hilo kama Haiti na El Salvador zinategemea pakubwa fedha zinazotokana na wafanyakazi wao wanaotumwa huko Marekani. Hii ni katika hali ambayo Trump si tu kuwa anafanya kila awezalo ili kusitisha chanzo hicho cha mapato bali anawadhalilisha watu hao kwa kuzitusi kuwa ni shimo la kinyesi nchi za Kiafrika na zile za Amerika ya Latini.

Hii ni katika hali ambayo tangu mwanzoni mwa karne hii Marekani imekuwa na ushindani wa kisiasa na kiuchumi kati yake na Russia, China na Umoja wa Ulaya; suala ambalo limepelekea kupungua ushawishi wa Washington katika eneo hilo huku nchi hizo zikiimarisha satwa yao katika kambi hiyo ya udhibiti wa zamani wa Marekani. Uuzaji silaha wa Russia, huku China ikiuza bidhaa kwa bei ya chini na wakati huo huo nchi za Ulaya zikitoa mikopo inayohitajika kumeandaa mazingira ya kujiimarisha nchi hizo huko Amerika ya Latini. Ni wazi kuwa harakati hizo zimeisababishia Marekani wasiwasi mkubwa.
Kwa msingi huo Rex Tillerson ameanza ziara yake katika eneo hilo kwa kutoa madai kwamba Russia inaingilia masuala ya uchaguzi huko Mexico na wakati huo huo kutahadharisha kuhusu eti hatua za kikoloni za China. Marekani inatoa madai hayo huku yenyewe kwa zaidi ya miaka 150 sasa imekuwa ikiingilia masuala ya uchaguzi katika nchi hizo za Amerika ya Latini; huku ikipora maliasili za nchi hizo kwa njia ya ukoloni na hivi sasa pia inayatia hatarini masuala ya wahajiri na muundo wa kiuchumi na kijamii wa nchi hizo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Vladimir Teriokhin Mhariri wa gazeti la Latin America akasema kuwa: Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwanza alipasa kutazama kwenye kioo na kushuhudia sura halisi ya ubeberu kabla ya kuzua madai hayo yasiyo na msingi dhidi ya Russia.