Feb 06, 2018 02:45 UTC
  • China yapinga stratijia mpya ya Marekani ya silaha za nyuklia

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China amesema nchi yake inapinga stratijia ya mpya ya Marekani ya silaha za nyuklia iliyotangazwa Ijumaa

Ren Guoqiang, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China amewataka watawala wa Marekani waachane na zile fikra za zama za vita baridi na watekeleze majukumu yao kuhusu kuangamiza silaha hatari za nyuklia. Amesema China imekuwa ikijizuia kueneza na kusambaza silaha za nyuklia na ina kiwango cha chini kabisa cha silaha hizo kwa ajili ya usalama wa taifa.

Siku ya Ijumaa  utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani ulitangaza sera mpya za nyuklia katika fremu ya 'Tathmini ya Hali ya Nyuklia-NPR.' Kwa mujibu wa sera hii mpya ya kistratijia, utawala wa Trump utaendeleza sehemu kubwa ya sera za nyukli za Marekani zilizotumika wakati wa utawala uliotangulia wa Barack Obama sambamba na kuchukua msimamo mkali na wenye uhasama zaidi kuhusu Russia. Aidha utawala wa Trump unasisitiza kuimarisha zaidi maghala ya silaha za nyuklia za Marekani. Hali kadhalika katika tathmini hiyo, China na Russia zimetajwa kuwa tishio kwa Marekani na hivyo imetangazwa haja ya kukabiliana na nchi hizo mbili.

Aidha sera mpya ya Marekani ya silaha za nyuklia inasisitiza uundwaji wa silaha ndogo ndogo za nyuklia ili kuzitumia katika vita hata kama upande wa pili hautatumia silaha za nyuklia. Huu ni mwelekeo mpya kwani Marekani hadi sasa imekuwa ikisisitiza kuwa silaha zake za nyuklia zinatumiwa kwa ajili ya kujihami iwapo upande wa pili utatumia silaha kama hizo.

Ren Guoqiang Msemaji wa Jeshi la China

Stephane Schwartz mtaalamu wa silaha za nyuklia anasema: "Wasiwasi mkubwa unahusiana na kuenea wigo wa silaha za nyuklia na hatua hii ya Marekani itapelekea uwezekano wa kutumiwa silaha za nyuklia kuongezeka zaidi."

Serikali ya China imesema stratijia mpya ya nyuklia ya Trump ni muendelezo wa vita baridi wakati kulipokuwa na mashindano ya silaha na kutegemea silaha za maangamizi ya umati katika kujihami. Aidha China imesema sera za nyuklia za Trump zinaonyesha namna Marekani inavyofadhilisha kutumia nguvu za kijeshi kutatua matatizo badala ya kutegemea ushirikiano. Inavyoelekea ni kuwa, Marekani sasa imeazimia kuimarisha maghala yake ya silaha na makombora ya nyuklia. Ni kwa sababu hii ndio maana China ikatangaza bayana kupinga sera mpya za kujitanua kijeshi Marekani na ikataka kuwepo ushirikiano wa kiraifiki baina ya mataifa ya dunia sambamba na kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi.

Ghala la silaha za nyuklia za Marekani

Anatoly Antonov, Balozi wa Marekani nchini Russia naye anasema: "Marekani kwa kuziweka China na Russia katika kambi ya maadui inataka kutumia kisingizo hicho kuimarisha bajeti ya kijeshi na uwezo wake wa silaha za nyuklia. Wanataka kutumia matrilioni ya dola katika  sekta yao ya kijeshi."

China inafahamu vyema kuwa lengo la Marekani ni kuchochea mashindano ya silaha za nyuklia na kuibua hali iliyokuwepo zama za vita baridi wakati wa utawala wa Shirikisho la Sovieti. Pamoja na kuwepo uchochezi huo, China na Russia zimeonyesha nia njema na zinasisitiza kuwa haziko tayari kuhatarisha usalama wa dunia kwa kuingia katika mchezo wa Marekani wa mashindano ya silaha.

Tags