Vita dhidi ya Uislamu katika michezo ya Olimpiki, Korea Kusini!
https://parstoday.ir/sw/news/world-i40189-vita_dhidi_ya_uislamu_katika_michezo_ya_olimpiki_korea_kusini!
Vita na hujuma dhidi ya Uislamu inaonekana sasa kushamiri zaidi na kuingia katika michezo ya kimataifa.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Feb 10, 2018 16:35 UTC
  • Vita dhidi ya Uislamu katika michezo ya Olimpiki, Korea Kusini!

Vita na hujuma dhidi ya Uislamu inaonekana sasa kushamiri zaidi na kuingia katika michezo ya kimataifa.

Vyombo vya habari vya Korea Kusini kunakofanyika michezo ya kipindi cha baridi ya Olimpiki vimeripoti kuwa, nchi hiyo imefuta mpango wa kujenga eneo la ibada ya Swala kwa ajili ya wanamichezo Waislamu kutokana na mashinikizo na malalamiko ya makundi yanayopinga Uislamu.

Gazeti la Korea Times limeandika kuwa, utawala wa mji wa Gangneung ambao ni miongoni mwa miji kunakofanyika michezo hiyo, umefuta mpango wa kutayarisha maeneo ya Swala kwa wanamichezo Waislamu baada ya malalamiko ya kundi linalopinga dini ya Uislamu.

Gazeti hilo limeripoti kuwa, kundi hilo linajiita Jumuiya ya Harakati Dhidi ya Uislamu. Kundi hilo pia limeitaka serikali ya Korea Kusini kuwa macho mbele ya eti harakati za Kiislamu na athari zake kwa mji huo na nchi nzima ya Korea Kaskazini.

Wanamichezo wa Iran, Pyeongchang nchini Korea Kusini

Kundi hilo lilianza harakati zake dhidi ya Uislamu nchini Korea Kusini baada ya kutolewa habari ya kuanza kujengwa maeneo ya Swala kwa ajili ya wanamichezo Waislamu mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Januari.

Michezo ya Olimpiki ya kipindi cha baridi ilizunduliwa rasmi jana Ijumaa katika mji wa Pyeongchang nchini Korea Kusini na itaendelea hadi tarehe 25 mwezi huu wa Februari.