UNICEF yatahadharisha kuhusu kutumiwa watoto kama askari vitani
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetahadharisha kuhusiana na suala la kutumiwa watoto kama askari vitani katika maeneo mbalimbali duniani.
Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimapatiafa ya kupambana na kutumiwa watoto vitani iliyoadhimishwa jana Jumatatu imeeleza kwamba, thekluthi moja ya watoto wanaotumiwa kama askari vitani katika maeneo mbalimbali duniani wanapatikana barani Afrika.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, katika mwaka uliopita wa 2017, jumla ya watoto 250,000 walitumiwa kama askari vitani katika maeneo mbalimbali duniani yanayoshuhudia vurugu na machafuko.
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza pia kwamba, nchi ya Sudan Kusini ambayo inashuhudia vita na mapigano ya wenyewe kwa wenywe kwa zaidi ya miaka minne sasa ndio inayokabiliwa zaidi na tatizo la kuwatumia watoto kama askari vitani.
Sehemu nyingine ya ripoti hiyo ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) imebainisha kwamba, katika nchi 20 duniani watoto wamekuwa wakilazimishwa kwenda vita, kufanya ujasuzi au kutekeleza operesheni za kujitolea muhanga na wamekuwa wakiishi kama wanajeshi katika makundi kama ya Boko Haram huko Nigeria na Sudan Kusini.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeeleza mpango wake wa kuwalea upya watoto ambao wameathirika na kuwa wahanga wa kutumiwa kama askari vitani na kupata madhara makubwa ya kisaikolojia.