Mgombea Mwislamu wa umeya, Marekani atishiwa kifo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i40405-mgombea_mwislamu_wa_umeya_marekani_atishiwa_kifo
Mgombea wa kike anayewania kuwa meya wa kwanza Mwislamu nchini Marekani amesema ametishiwa kuuawa kama ataendelea kuwa mgombea katika kinyang'anyiro hicho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 15, 2018 12:35 UTC
  • Mgombea Mwislamu wa umeya, Marekani atishiwa kifo

Mgombea wa kike anayewania kuwa meya wa kwanza Mwislamu nchini Marekani amesema ametishiwa kuuawa kama ataendelea kuwa mgombea katika kinyang'anyiro hicho.

Regina Mustafa, anayewania umeya wa mji wa Rochester katika jimbo la Minnesota amesema kundi la "Militia Movement" limetoa taarifa mtandaoni likitishia kumuua.

Mustafa amesema kuwa vitisho hivyo haviwezi kumzuia kugombea nafasi hiyo lakini vinapaswa kupewa uzito na mazingatio. Mwanamke huyo Muislamu amesema mtu yeyote hapaswi kuhisi vitisho wakati anapotaka kugombea nafasi ya kuchaguliwa kwa ajili ya kutumikia taifa lake.

Baraza la Mahusiano ya Waislamu na Marekani (CAIR) limelaani vitisho hivyo dhidi ya mgombea Mwislamu wa kiti cha umeya wa mji wa Rochester na kuitaka polisi ya Marekani kuchunguza suala hilo.

Taarifa iliyotolewa na CAIR imesema polisi ya Federali inapaswa kuchunguza vitisho hivyo vilivyotolewa dhidi ya watu wa jamii za waliowachache wanaotaka kutumia haki yao ya kushiriki kwenye masuala ya kisiasa.

Makundi ya kibaguzi yameshika kasi Marekani baada ya Trump kushika hatamu za uongozi

Gazeti la Star Tribune la Marekani limeandika kuwa, Regina Mustafa amekuwa akishambuliwa kwa maneno na wafuasi wa makundi ya kibaguzi nchini Marekani.

Mashambulizi na hujuma dhidi ya jamii za waliowachache hususan Waislamu na wahajiri yameongezeka nchini Marekani kutokana na siasa za Rais wa sasa wa nchi hiyo, Donald Trump za kuwapiga vita Waislamu na wahajiri.