Russia yapigia veto muswada wa Uingereza dhidi ya Iran kuhusu Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/world-i40917-russia_yapigia_veto_muswada_wa_uingereza_dhidi_ya_iran_kuhusu_yemen
Muswada wa azimio lililo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliopendekezwa na Uingereza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, umekwamishwa na kura ya veto ya Russia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 26, 2018 23:24 UTC
  • Russia yapigia veto muswada wa Uingereza dhidi ya Iran kuhusu Yemen

Muswada wa azimio lililo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliopendekezwa na Uingereza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, umekwamishwa na kura ya veto ya Russia.

Jana Jumatatu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha kujadili miswada miwili kuhusu Yemen.

Muswada wa kwanza umependekezwa na Uingereza kwa ajili ya kuiweka Iran chini ya mashinikizo kupitia madai ya uongo ya kwamba Tehran inatuma silaha nchini Yemen. Hata hivyo muswada huo umeshindwa kufurukuta mbele ya kura ya veto ya Russia.

Uingereza haioni mateso ya wananchi wa Yemen wala jinai zinazofanywa na Saudia bali inachomwa zaidi wakati Wayemen wanaodhulumiwa wanapoamua kulipiza kisasi japo kidogo

 

Muswada wa pili umependekezwa na Russia lakini umehusiana tu na kurefushwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Yemen hadi mwezi Februari 2019. Muswada huo umepita kwa kura zote za wanachama 15 wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Uingereza imeshirikiana na Marekani na Ufaransa kuandaa muswada wa azimio la kuishinikiza Iran.

Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia kwa kusaidiwa na Imarati, Marekani, Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel ilianzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya nchi maskini ya Kiislamu ya Yemen na hadi hivi sasa madola hayo ya kibeberu yanaizingira nchi hiyo ya Kiarabu kutokea angani, ardhini na baharini. Hadi hivi sasa vita hivyo vya kikatili vinavyoongozwa na Saudia dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Yemen vimeshaua na kujeruhi makumi ya maelfu ya watu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya wengine.

Mara kwa mara viongozi wa Yemen wanasema kuwa, nguvu zao za kijeshi ni za ndani kikamilifu, na wala Iran haijawahi kuwapa silaha zozote. Wanasema madai yote hayo dhidi ya Iran ni sehemu ya njama za madola hayo vamizi ya kuficha kushindwa kwao katika vita vya Yemen.