Kim Jong-un ataka kupanuliwa mahusiano na Korea Kusini haraka
Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini sambamba na kufurahishwa na hatua ya Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini ya kumtuma mjumbe wake maalumu mjini Pyongyang, ametaka kuboreshwa haraka mahusiano ya nchi mbili.
Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini ameyasema hayo kwa mnasaba wa safari ya ujumbe wa Korea Kusini nchini mwake ambapo amesema kuwa, Pyongyang inaunga mkono kikamilifu ustawishaji wa haraka wa mahusiano kati ya Korea mbili sambamba na kufunguliwa ukurasa mpya wa kihistoria katika mahusiano hayo. Kadhalika Kim Jong-un ametaka kupunguzwa mizozo ya kijeshi katika eneo la Rasi ya Korea na badala yake kuendelezwa mazungumzo na Korea Kusini.
Chong Yi-Yong, mjumbe maalumu wa Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini alifanya safari mjini Pyongyang Jumatatu ya jana ambapo alisema kuwa akiwa Korea Kaskazini atajadiliana na viongozi wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya silaha za nyuklia.
Katika miezi ya hivi karibuni Korea Kusini na Korea Kaskazini zimekuwa na mahusiano mazuri tangu kulipojiri mazungumzo yaliyoishawishi Pyongyang kutuma wanamichezo wake kwa ajili ya kushiriki michuano ya msimu wa baridi iliyomalizika hivi karibuni.