Makumi ya watu wapoteza maisha baada ya ndege kuanguka Kathmandu, Nepal
Ndege ya abiria iliyokuwa imebaba watu 71 kutoka Bangladesh imeanguka wakati ikitua katika uwanja wa ndege wa Kathmandu, mji mkuu wa Nepal ambapo taarifa zainasema makumi ya watu wamefariki.
Idadi kamili ya waliofariki haijulikani lakini msemaji wa Jeshi la Nepal Brigedia Jenerali Gokul Bhandari amesema watu 50 wamepoteza maisha katika ajali hiyo ya Jumatatu asubuhi.
Ndege hiyo aina ya Bombardier Dash 8 iliyotengenezwa Canada inamilikiwa na Shirika la Ndege la US-Bangla na hadi sasa haijulikani ni kwa nini ilianguka wakati ikijaribu kutua.
Taarifa zinasema ndege hiyo iliuzunguka uwanja wa ndege wa Kathmandu mara mbili kabla ya kupewa idhini ya kutua. Wakuu wa uwanja wa ndege wanasema ndege hiyo ilikuwa imepewa idhini ya kutua katika runway ya upande wa kusini lakini ikaelekea upande wa kaskazini kabla ya kuanguka.
Waziri Mkuu wa Nepal KP Sharma Oli ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga wa ajali hiyo na kutaka uchunguzi wa haraka ufanyike.