Kasisi wa Marekani kupandishwa kizimbani Uturuki kwa tuhuma za ugaidi
Kasisi mmoja raia wa Marekani huenda akahukumiwa kifungo cha miaka 35 jela nchini Uturuki iwapo atapatikana na hatia katika tuhuma za ugaidi na ujasusi zinazomkabili.
Televisheni ya serikali ya Anadolu nchini Uturuki imeripoti kuwa, wakuu wa mashitaka katika mji wa Izmir, magharibi mwa nchi wanaitaka mahakama imhukumu kifungo hicho Andrew Brunson, kasisi wa Marekani anayedaiwa kushirikiana na mtandao wa mwanachuoni wa Uturuki aliyeko Marekani, Fethullah Gulen na wapiganaji wa Kikurdi kusababisha machafuko nchini Uturuki na kuligawa taifa hilo.
Hata hivyo haijabainika lini kesi dhidi ya mchungaji huyo wa Kikristo wa Marekani itaanza kusikilizwa.
Brunson, ambaye ni mkazi wa eneo la North Carolina na ambaye ameishi nchini Uturuki kwa takriban miaka 20, alikamatwa mwezi Julai mwaka 2016, baada ya jaribio la mapinduzi lililofeli. Marekani imekuwa ikiitaka serikali ya Ankara imuachie huru kiongozi huyo wa Kikristo.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alitishia kwamba, ikiwa Marekani itaendelea kukataa ombi la Ankara la kumrejesha nyumbani Fethullah Gülen ambaye anatafutwa na Uturuki, basi nchi hiyo nayo italazimika kuchukua hatua za kukabiliana na Washington.
Hadi sasa Ankara imeshaikabidhi Washington washukiwa 12 wa ugaidi kwa mujibu wa ombi la Marekani, lakini Washington imekataa kumkabidhi Fethullah Gülen anayetuhumiwa kuratibu mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli tarehe 15 Julai 2016 nchini Uturuki.