Mcheza filamu za ngono atishiwa usalama wake kwa kumsakama Donald Trump
(last modified Mon, 26 Mar 2018 07:50:08 GMT )
Mar 26, 2018 07:50 UTC
  • Mcheza filamu za ngono atishiwa usalama wake kwa kumsakama Donald Trump

Mcheza filamu chafu za ngono ambaye amepata umaarufu kwa kufichua kwamba aliwahi kutembea kimwili kwa miezi kadhaa na rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa amepokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana wakimtaka aache kumsakama Trump.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Stormy Daniels kwa mara nyingine alisema jana katika mahojiano na televisheni moja kwamba alikuwa na uhusiano wa kijinsia na Donald Trump na alipotaka kuiuza taarifa yake hiyo kwa jarida moja kwa thamani ya dola 15,000, alitishiwa usalama wake na wa binti yake akitakiwa anyamaze kimya.

Donald Trump na mkewe Melania Trump

 

Amesema, alikuwa na uhusiano wa kijinsia wa miezi kadhaa na Rais Donald Trump mwaka 2006, licha ya kwamba wakati huo Trump alikuwa tayari ameshamuoa mke wake wa hivi sasa, Melania Trump.

Hata hivyo Ikulu ya Marekani, White House imekuwa ikikanusha madai hayo licha ya Stormy Daniels kusisitiza mara kwa mara kwamba alikuwa na uhusiano wa kijinsia nje ya ndoa na rais huyo wa Marekani tena kwa miezi kadhaa.

Alipoulizwa je ana video au picha au b-pepe au ujumbe wa maandishi wa kuthibitisha madai yake hayo, Daniels amesema: "Siwezi kusema chochote kuhusu suala hilo kwa hivi sasa."