Kiongozi wa Korea Kaskazini afanya safari ya kinyemela China?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i42260-kiongozi_wa_korea_kaskazini_afanya_safari_ya_kinyemela_china
Duru za habari zimefichua kuwa, yumkini kiongozi wa Korea Kaskazini amefanya safari ya kificho nchini China.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 27, 2018 07:29 UTC
  • Kiongozi wa Korea Kaskazini afanya safari ya kinyemela China?

Duru za habari zimefichua kuwa, yumkini kiongozi wa Korea Kaskazini amefanya safari ya kificho nchini China.

Tovuti ya habari ya Bloomberg jana Jumatatu ilinukuu vyanzo vitatu vya habari ambavyo havijataka kutajwa jina, vikisema kuwa Kim Jong-un amesafiri China ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu achukue usukani mwaka 2011. Hata hivyo duru hizo za habari hazijatoa maelezo zaidi kuhusu ripoti hizo.

Kadhalika shirika la habari la Japan la Kyodo liliripoti Jumapili iliyopita kwamba kiongozi huyo wa Korea Kaskazini yuko nchini China, na kwamba alisafiri kwa treni kupitia mji wa Dandong, katika mpaka wa China.

Kanda ya video ya shirika la Nippon News Network la Japan imeonyesha treni yenye kichwa cha rangi ya kijani na mabogi yenye rangi ya manjano ikiingia China, garimoshi linalofanana na lile lililotumiwa na babake, Kim Jong-il mwaka 2011, aliposafiri kwenda Beijing.

Ramani inayoonyesha Peninsula ya Korea

Hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini ilisema Korea Kaskazini imetuma ujumbe wa kukubali suala la kufanyika mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Korea mbili hizo tarehe 29 mwezi huu wa Machi katika kijiji cha Panmunjom kilichoko katika mpaka wa nchi hizo jirani. 

Mahusiano kati ya Pyongyang na Seoul yamekuwa yakiboreka tangu kulipojiri mazungumzo ya pande mbili kwa ajili ya kuishawishi Korea Kaskazini ishiriki katika michuano ya olimpiki katika msimu wa baridi kali nchini Korea Kusini.