Guterres: Kufukuzwa wanadiplomasia wa Russia kunakumbusha kipindi cha Vita Baridi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusiana na hatua ya baadhi ya nchi za Magharibi ya kuwafukuza wanadiplomasia wa Russia na kusema hali hiyo inakumbusha kipindi cha Vita Baridi.
Antonio Guterres amewaambia waandishi habari mjini New York kwamba, kufukuzwa kwa wanadiplosia wa Russia katika nchi hizo kunaweza kuzidisha mivutano na mapigano.
Zaidi ya nchi 25 za Magharibi ikiwemo Marekani na Uingereza zimewafukuza wanadiplomasia karibu 150 wa Russia kwa kisingizio cha kuonesha mshikamano wao na Uingereza baada ya London kudai kuwa, Moscow ilihusika na jaribio la kutaka kumuua jasusi wake wa zamani, Sergei Skripal na binti yake, Yulia katika eneo la Salisbury huko kusini mwa London.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amezungumzia mkutano ujao baina ya viongozi wa Korea Kaskazini na Kusini na kusema: China ina nafasi muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa Peninsula ya Korea.
Juzi tarehe 27 Machi Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un alikutana kwa mara ya kwanza kabisa na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing ambako pande mbili zilijadili masuala ya Peninsula ya Korea.