Wimbi la upinzani wa kuuziwa silaha Saudi Arabia huko Ufaransa
Malalamiko ya kutaka kusitishwa kuuziwa silaha Saudi Arabia yameshadidi nchini Ufaransa sambamba na safari ya Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia katika nchi hiyo ya bara Ulaya.
Bin Salman ambaye juzi aliwasili mjini Paris Ufaransa kwa ziara rasmi nchini humo, alikaribishwa kwa maandamano yanayoitaka serikali ya Rais Emmanuel Macron isitishe kuuzuia silaha utawala wa Aal Saud ambao umekuwa ukifanya mauaji dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen. Baadhi ya Wabunge wa chama cha Rais Macron wamewasilisha ombi rasmi la kutaka kufanyika uchunguzi kuhusiana na uhalali wa kuuzuia silaha muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen. Kabla ya hapo pia, baadhi ya asasi na jumuiya za kimataifa zilikuwa zimetoa wito wa kusitisha kuuziwa silaha Saudi Arabia na waitifaki wake katika vita dhidi ya Yemen. Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Sweden ndio wauzaji wakubwa wa silaha kwa Saudi Arabia na washirika wake.
Hii ni katika hali ambayo, akthari ya nchi hizo zimekuwa zikijitokeza katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa na kupiga nara za kupinga vita na kupigia upatu haki za binadamu. Kwa muktadha huo, hatua yao ya kuuzia silaha utawala wa Aal Saud unaotenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi wa Yemen ni ithbati tosha kwamba, madai yao ya kupinga vita na kutetea haki za binadamu ni hadaa na urongo mtupu. Malalamiko dhidi ya kuiuzia silaha Saudi Arabia yameshtadi katika hali ambayo, utawala wa Riyadh na washirika wake wakipata uungaji mkono wa Marekani na Magharibi walianza kuishambulia kijeshi Yemen Machi 26 mwaka 2015 ambapo matokeo yake ni kuuawa zaidi ya raia elfu 14 na kujeruhiwa wengine elfu kumi.
Aidha kubomolewa miundo mbinu ya Yemen na kuzingirwa kila upande nchi hiyo na Saudi Arabia kumepelekea kuibuka uhaba mkubwa wa dawa na chakula sambamba na mfumuko wa maradhi mbalimbali kikiwemo kipindupindu. Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International kitengo cha Mashariki ya Kati unaonyesha kuwa: Kuuziwa silaha kusiko kwa kuwajibika muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kumewasababishia madhara mengi wananchi madhulumu wa Yemen. Saudi Arabia hainunui silaha kwa ajili tu ya kuzitumia katika vita huko Yemen, bali kulipatia kundi la kigaidi la Daesh ni lengo jingine la Riyadh la kutumia mamilioni ya dola kwa ajili ya kununua silaha na zana za kijeshi. Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti wa masuala ya silaha ni kuwa, sehemu kubwa ya silaha za kundi la kigaidi la Daeshzinatoka Marekani na Saudi Arabia.
Licha ya malalamiko yote hayo, lakini Saudi Arabia na waitifaki wake wameendelea kununua silaha na zana za kijeshi huku Marekani na washirika wake nao wakiyapuuza malalamiko ya ndani na ya kimataifa yanayopinga kuuziwa silaha utawala wa Aal Saud. Sergey Syberibov, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuwa, Marekkani na Uingereza zinapata faida nono kutokana na kuendelea vita vya Yemen.
Inaonekana kuwa, malalamiko yanayoendelea huko Ulaya na Marekani ya kupinga kuuziwa silaha Saudia hayawezi kuwafanya wauzaji na wanunuzi wa silaha hizo kubadilisha misimamo yao hasa kwa kutilia maanani kwamba, maslahi yao ya kiuchumi yamo katika kuuza na kununua silaha na kuimarisha uwepo wao katika eneo hili la Mashariki ya Kati. Katika upande mwingine, lobi tajiri za Kisaudia nazo daima zimekuwa zikifanya harakati ili kuandaa mazingira ya kununuliwa silaha nyingi kadiri inavyowezekana kutoka Ulaya na Marekani.
Pamoja na hayo, kuongezeka wimbi la malalamiko ni ithbati tosha ya kutoridhishwa fikra za waliowengi ulimwenguni na siasa za kindumakuwili za madola ya Magharibi. Katika mazingira kama haya, kuendelea serikali husika kupuuza matakwa ya fikra za waliowengi hasa kwa kutilia maanani taathira yake kwa vijana na makundi ya kiraia ni jambo ambalo katika kipindi cha muda mrefu linaweza kupelekea kupanuka wigo wa malalamiko hayo na kuziweka katika mashinikizo makubwa siasa za nchi zinazojihusisha na biashara hiyo ya silaha.