Ripoti: Wahajiri wa Kiafrika walioko US wamesoma kuliko Wamarekani wenyewe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43606-ripoti_wahajiri_wa_kiafrika_walioko_us_wamesoma_kuliko_wamarekani_wenyewe
Utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew umeonyesha kuwa, kuna mwanya mkubwa wa kiwango cha elimu kati ya wahajiri wa Kiafrika wanaoishi Marekani na raia wa asili wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2018 22:01 UTC
  • Ripoti: Wahajiri wa Kiafrika walioko US wamesoma kuliko Wamarekani wenyewe

Utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew umeonyesha kuwa, kuna mwanya mkubwa wa kiwango cha elimu kati ya wahajiri wa Kiafrika wanaoishi Marekani na raia wa asili wa nchi hiyo.

Ripoti ya utafiti huo iliyotolewa jana Jumanne imeonyesha kuwa, aghalabu ya wahajiri wa Kiafrika hususan wanaotoka katika eneo la chini ya Jangwa la Sahara wanaoishi nchini Marekani wana kiwango cha juu cha elimu kuliko Wamarekani wenyewe.

Utafiti huo umesema kuwa, asilimi 69 ya wahajiri hao wa Kiafrika walioko nchini Marekani wana elimu ya taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, ukilinganisha na idadi kubwa ya Wamarekani wenyewe ambao hawana viwango vya juu vya elimu kama hivyo.

Aidha utafiti huo umebainisha kuwa, ni kutokana na kiwango chao cha juu cha elimu ndipo aghalabu ya wahajiri hao wameajiriwa katika taasisi na mashirika mbali mbali nchini humo, huku akthari ya vijana wa Kimarekani wakikosa ajira kutokana na viwango vya chini vya elimu.

Polisi nchini Marekani wakimpa kichapo Mmarekani mwenye asili ya Afrika

Ripoti ya Kituo cha Utafiti cha Pew inasema kuwa, asilimi 92 ya wahajiri wa Kiafrika nchini Marekani wenye viwango vya juu vya elimu wameajiriwa kutokana na masomo na tajriba zao.

Hii ni katika hali ambayo, ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wahajiri zimeongezeka kwa kiasi kikubwa nchini Marekani tangu aingie madarakani Rais Donald Trump.