Siasa za Trump zaendelea kuchochea ukati dhidi ya Waislamu Marekani
Uchunguzi uliofanyika hivi karibuni umeonesha kuwa, kuongezeka kwa ukatili na jinai zinazotokana na chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani kuna mfungamano na siasa za Rais wa sasa wa nchi hiyo, Donald Trump.
Matokeo ya uchunguzi huo ambayo yamechapishwa na Council on American–Islamic Relations (CAIR) yanaonesha kuwa, mwaka 2017 kulisajiliwa jinai 300 zilizosababishwa na chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani, kiwango ambacho kimeongezeka kwa asilimia 44 ikilinganishwa na mwaka 2016.
Mkurugenzi Mtendaji wa CAIR, Nihad Awad amesema kuwa, matukio yanayowalenga Waislamu yameendelea kushika kasi na kuongezeka yakiambatana na ukatili na kwamba yamawalenga zaidi watoto, vijana na familia za Kiislamu.
Mawakili wa jumuiya ya Waislamu nchini Marekani ya CAIR wanasema kuwa, matukio mengi ya hujuma dhidi ya Waislamu yana mfungamano na wakala na idara za Federali ya Marekani na kwamba yanaakisi uhasama usio na kifani wa maafisa wa serikali dhidi ya wafuasi wa dini ya waliowachache.
Hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu yake vimeongezeka sana nchini Marekani baada ya Donald Trump kuchaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo.