Russia yapinga matamshi ya Trump, Macron kuhusu makubaliano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43692-russia_yapinga_matamshi_ya_trump_macron_kuhusu_makubaliano_ya_jcpoa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amepinga matamshi yaliyotolewa na Marais wa Marekani na Ufaransa kuhusu suala la kufanyiwa mabadiliko makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 26, 2018 23:14 UTC
  • Russia yapinga matamshi ya Trump, Macron kuhusu makubaliano ya JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amepinga matamshi yaliyotolewa na Marais wa Marekani na Ufaransa kuhusu suala la kufanyiwa mabadiliko makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Maria Zakharova amekosoa matamshi yaliyotolewa na Donald Trump na Emmanuel Macron kuhusu makubaliano ya nyuklia ya nchi za kundi la 5+1 na Iran na kusisitiza kuwa haiwezekani kufanyika mabadiliko ya aina yoyote katika makubaliano hayo. 

Akijibu taarifa iliyotolewa kwa pamoja na Marais wa Marekani na Ufaransa, Zakharova amesema kuwa makubaliano hayo yana mlingano na yamezingatia maslahi ya pande zote husika. 

Rais wa Ufaransa anapendekeza kulindwa makubalianio ya sasa ya nyuklia kati ya Iran na nchi zita wanachama katika kundi la 5+1 sambamba na kuzidishwa vipengee vingine katika makubaliano hayo.

Macron na Trump

Kwa upande wake Rais Donald Trump wa Marekani anadai kuwa makubaliano hayo yanadhamini maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pekee na ametoa wito wa kufanyiwa mabadiliko kwa maslahi ya Washington.

Makubaliano ya nyuklia yaliyotiwa saini na Iran kwa upande mmoja na nchi za Uingereza, Ufaransa, Marekani, Russia, China na Ujerumani kwa upande mwingine yalianza kutekelezwa Januari mwaka 2016. Hata hivyo Marekani ikiwa mmoja kati ya waliotia saini makubaliano hayo imekuwa ikipindisha na kukiuka utekelezaji wake.