Hatimaye Korea Kaskazini yakubali kuangamiza makombora yake ya balestiki
Serikali ya Korea Kaskazini sambamba na kukubali kuangamiza makombora yake ya kutoka bara hadi bara ya balestiki, imekubali pia kutumwa wataalamu wa kimataifa kwenda kukagua taasisi za nyuklia za nchi hiyo.
Kufuati ripoti hiyo, gazeti la Sahi la nchini Japan limedai kuwa kundi moja la wataalamu wa silaha za nyuklia kwa kushirikiana na wataalamu wa shirika la ujasusi la Marekani CIA wamewasili Korea Kaskazini kwa ajili ya kuchunguza vinu vya nyuklia vya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ya Korea Kaskazini pia na kwa mara ya kwanza imekubali wataalamu wa kimataifa kukagua taasisi zake za nyuklia.
Kabla ya hapo pia Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini alitangaza kuwa katika miezi kadhaa ijayo Pyongyang itafunga maeneo ya kuzalishia silaha za nyuklia sambamba na kuwakaribisha wataalamu na waandishi wa habari kuweza kutembelea maeneo hayo. Katika mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un viongozi hao walitia saini makubaliano ya kutokomeza kikamilifu na silaha za nyuklia katika eneo la Korea, suala ambalo lilipongezwa pia na dunia nzima.
Katika hatua nyingine Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un amesisitiza kwamba nchi yake itafungamana na makubaliano ya kutokomeza silaha za nyuklia katika eneo la Korea. Kim Jong-un ameyasema hayo Alkhamisi ya leo alipokutana na Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China mjini Pyongyang na kusisitiza kuwa, mabadiliko chanya yaliyoshuhudiwa katika eneo hilo, yamekuwa na faida kubwa katika njia ya kuelekea amani.