Russia: Iwapo Marekani itajitoa katika JCPOA, itabidi iwekewe vikwazo
-
Vladimir Yermakov
Afisa mmoja wa Russia amesisitiza kuwa, kama Marekani itajitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, itabidi iwekewe vikwazo vya kimataifa.
Vladimir Yermakov, mkuu wa ofisi ya kuzuia uenezaji na udhibiti wa silaha ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia alisema hayo jana na kuongeza kuwa, kama Marekani itayavunja mapatano hayo ya kimataifa ambayo yamepasishwa pia na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Washington ndiyo itakayopata pigo.
Ameongeza kuwa, itabidi Marekani iwekewe vikwazo vya kimataifa kama itayavunja mapatano ya JCPOA.
Vile vile amesema, iwapo Marekani itajitoa kwenye mapatano hayo, Russia itaandaa muswada ya kuyafanya yaendelee kuwepo bila ya Marekani, bali baina ya Iran na nchi za Ulaya pamoja na Russia na China.
Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameongeza kuwa, hakuna vikwazo vyovyote vipya vitakavyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kwa maana ya kwamba iwapo Marekani itajitoa katika mapatano ya JCPOA, Baraza la Usalama haliweka kikwazo chochote kile dhidi ya Iran.
Muda aliojiwekea rais wa Marekani ya kuamua ima kubakia au kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ambayo Washington ilishiriki kikamilifu kuyafanikisha, ni tarehe 12 mwezi huu wa Mei.