Korea Kaskazini: Marekani inachafua anga ya mazungumzo kwa kueneza uwongo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44114-korea_kaskazini_marekani_inachafua_anga_ya_mazungumzo_kwa_kueneza_uwongo
Wiki chache kabla ya kufanyika mazungumzo yanayosubiriwa kwa shauku kuu kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, Pyongyang imekosoa vikali kile ilichokitaja kama upotoshaji wa makusudi wa Washington, kwamba sera za Trump za kushadidisha vikwazo na mashinikizo ya kisiasa dhidi ya nchi hiyo ndizo zilizopelekea Korea Kaskazini kukubali kwenda katika meza ya mazungumzo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 06, 2018 07:32 UTC
  • Korea Kaskazini: Marekani inachafua anga ya mazungumzo kwa kueneza uwongo

Wiki chache kabla ya kufanyika mazungumzo yanayosubiriwa kwa shauku kuu kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, Pyongyang imekosoa vikali kile ilichokitaja kama upotoshaji wa makusudi wa Washington, kwamba sera za Trump za kushadidisha vikwazo na mashinikizo ya kisiasa dhidi ya nchi hiyo ndizo zilizopelekea Korea Kaskazini kukubali kwenda katika meza ya mazungumzo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini amesema mienendo ya namna hiyo ya kutoa madai ya upotoshaji ni ya hatari na inayoweza kuvuruga hatua chanya zilizofikiwa katika wiki za hivi karibuni katika Peninsula ya Korea.

Amesema Marekani kwa makusudi inaichokoza Korea Kaskazini wakati huu ambapo Peninsula ya Korea ipo mbioni kuelekea katika njia ya amani na maridhiano.

Kwa mujibu wa Pyongyang, uamuzi wa kukutana na Trump na pia kusimamisha majaribio ya silaha za nyuklia na makombora ya balestiki umefikiwa na kiongozi wa Korea Kaskazini mwenyewe, na wala sio kutokana na mashinikizo na vikwazo.

Kiongozi wa Korea Kaskazini na Rais wa Korea Kusini walipokutana hivi karibuni

Kwa mujibu wa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, sababu ya kusimamishwa majaribio ya silaha za nyuklia na makombora ya balestiki ya nchi yake ni kwamba, Pyongyang imeshakamilisha mradi huo na kwamba haina haja tena ya kuendelea nao. 

Kim na Trump wanatazamiwa kukutana ima mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi ujao wa Juni.