Kiongozi mkongwe wa upinzani (92) ashinda uchaguzi Malaysia
Kiongozi mkongwe wa upinzani ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Malaysia ameshinda uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo, kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Tume ya Uchaguzi, na kutamatisha utawala wa karibu miongo sita wa mrengo tawala wa Barisan Nasional.
Mrengo wa upinzani unaoongozwa na Dakta Mahathir Mohamad mwenye umri wa miaka 92, umeibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kuzoa wingi wa kura halali zilizopigwa katika uchaguzi huo.
Mrengo huo wa Pakatan Harapan umeshinda viti 115, katika hali ambayo chama au mrengo wa kisiasa unaozoa viti 112 Bungeni huwa umetimiza kigezo cha kuunda serikali.
Baada ya kutangazwa mshindi, Dakta Mahathir amewaambia waandishi wa habari kuwa, "Sisi hatutaki kulipiza kisasa, tunataka kuhuisha utawala wa sheria."

Kiongozi huyo mkongwe mwenye miaka 92 anatoka katika maisha ya kustaafu na kuja kuiongoza tena Malaysia, baada ya nchi hiyo hiyo kukabiliwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi na mfumkoa wa bei za bidhaa muhimu. Kadhalika anakuja kurithi mikoba ya Waziri Mkuu anayeondoka Najib Razak, ambaye amekuwa akiandamwa na kashfa mbali mbali za ufisadi.
Kufuatia ushindi wa mrengo wa upinzani wa Pakatan Harapan, serikali imetangaza kuwa leo Alkhamis na kesho Ijumaa zitakuwa siku za kitaifa za mapumziko.