Onyo la Korea Kaskazini kwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44594-onyo_la_korea_kaskazini_kwa_marekani
Katika radiamali ya matamshi ya viongozi wa Marekani dhidi ya Korea Kaskazini na kadhalika maneva ya anga ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini ametahadharisha kwamba, iwapo Washington itaendeleza mashinikizo yake dhidi ya Pyongyang kuhusu mpango wake wa nyuklia, basi nchi hiyo italazimika kuangalia upya kikao tarajiwa kati ya Trump na Kim Jong-un.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 17, 2018 07:52 UTC
  • Onyo la Korea Kaskazini kwa Marekani

Katika radiamali ya matamshi ya viongozi wa Marekani dhidi ya Korea Kaskazini na kadhalika maneva ya anga ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini ametahadharisha kwamba, iwapo Washington itaendeleza mashinikizo yake dhidi ya Pyongyang kuhusu mpango wake wa nyuklia, basi nchi hiyo italazimika kuangalia upya kikao tarajiwa kati ya Trump na Kim Jong-un.

Kim Kye-gwan, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, ameitaka Washington kuzungumza na  Pyongyang kwa nia ya kweli ili kuweza kufikiwa malengo stahiki ya pande mbili. Aidha katika kulalamikia hatua ya Marekani na Korea Kusini ya kufanya maneva ya kijeshi ya pande mbili, Korea Kaskazini imevunja mazungumzo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Jumatano ya jana kati ya jumbe za ngazi ya juu katika ngazi ya mawaziri baina ya Pyongyang na Seoul.

Kim Kye-gwan, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini

Mazungumzo kati ya Kim Jong-un na Rais Donald Trump wa Marekani yamepangwa kufanyika tarehe 12 Juni nchini Singapore. Korea Kaskazini imeyataja matamshi ya hivi karibuni ya viongozi wa Marekani akiwemo John  Bolton, Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani kuhusu kufungwa miradi ya nyuklia ya Pyongyang na wakati huo huo kufanyika maneva ya pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini, licha ya kuboreka uhusiano kati ya Korea mbili, kuwa ni ya uchochezi dhidi ya hatua za usalama na uthabiti wa Rasi ya Korea. Hivi karibuni Korea Kusini na Marekani zilianzisha maneva kubwa ya anga katika maji ya eneo la Korea.

John Bolton, Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani

Hii ni katika hali ambayo katika mkutano wao wa hivi karibuni, viongozi wa Korea mbili, walikubaliana kuendeleza juhudi za kudumisha usalama wa kudumu katika eneo hilo na kufikia mwishoni mwa mwaka huu waweze kuyabadili makubaliano ya amani ya pande mbili ya kuacha uhasama baina yao, kuwa mkataba wa amani kamili. Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa usalama wa Korea Kusini uko mikononi mwa Marekani ambayo ina askari elfu 40 ndani ya nchi hiyo ya Asia, nchi hiyo ya Magharibi imekuwa ikiishinikiza serikali ya Seoul udumishe ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili na Washingon. Suala muhimu ni hili kwamba, Marekani imekuwa ikionyesha kutopendelea kuona mgogoro wa Korea ukipatiwa ufumbuzi na ndio maana imekuwa ikitumia mzozo wa nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini kama wenzo wa kujiimarisha zaidi kijeshi dhidi ya taifa la China sambamba na kuibana zaidi nchi hiyo.

Marekani inajiimarisha zaidi kijeshi Korea Kusini kwa lengo la kuibana China

Katika hali ambayo Korea Kaskazini ilikuwa imelegeza misimamo yake kwa ajili ya kuelewana na kushirikiana zaidi na jinari yake Korea Kusini, kwa upande wake Marekani inavuruga mwenendo huo wa amani na hivyo kuhatarisha usalama wa eneo hilo zima. Lengo la Marekani kuhusu suala hilo ni kujaribu kuitwisha matakwa yake serikali ya Pyongyang. Gazeti la Minju Choson la Korea Kaskazini limeandika kwamba: "Rais Donald Trump wa Marekani ni mwenye mawazo ya zamani sana yaliyopitwa na wakati ambapo anadhani kwamba utatuzi wa masuala muhimu ya kimataifa unategemea mabavu hususan kuhusiana na kadhia ya kuimarisha usalama wa eneo la Korea. Ni wazi kuwa anafanya kosa kubwa la kisiasa." Mwisho wa kunukuu.

Ni hivi karibuni tu ambapo Kim Jong-un alikutana na Rais wa Korea Kusini

Aidha katika hali ambayo fikra za walio wengi nchini Korea Kusini zinaunga mkono utatuzi wa mgogoro uliopo kati ya nchi yao na Korea Kaskazini, viongozi wa Marekani hivi karibuni sambamba na kutoa mapendekezo kadhaa mapya kama vile kufunga na kuhamisha miradi ya nyuklia ya Pyongyang kwenda nje ya nchi hiyo, wamefanya njama ya kutia doa mwenendo wa utatuzi wa mizozo ya eneo. Hayo yanajiri huku Korea Kaskazini na kwa mujibu wa makubaliano iliyoyafikia na jirani yake Korea Kusini, imeamua kufunga maeneo yake ya kufanyia majaribio silaha za nyuklia ikiwa ni kuvutia uaminifu na juhudi za kuleta maelewano kati ya Korea mbili.

Leon Panetta, waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani ambaye amemuonya Trump

Katika uwanja huo, hivi karibuni Leon Panetta, waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani alisema: "Matamshi ya uhasama ya Trump kuilenga Korea Kaskazini, yanaongeza uwezekano wa kuzua vita eneo la mashariki mwa Asia na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu. Tunakabiliwa na vita vya nyuklia ambavyo vinaweza kusababisha maafa makubwa ya mamilioni ya watu. Nadhani tunapaswa kuchukua tahadhari na kutofanya pupa katika uwanja huo." Mwisho wa kunukuu. Alaa kullihaal, tajriba inaonyesha kwamba, mazungumzo ndio njia pekee ya kutatuliwa mgogoro wa Rasi ya Korea, mbali na mashinikizo ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini. Hata hivyo kutokana na tabia ya Marekani ya kupenda makubwa katika mwenendo wa mazungumzo hayo, ni wazi kuwa inataka kuitwisha Pyongyang mapendekezo ya upande mmoja, suala ambalo linapingwa vikali na viongozi wa Korea Kaskazini.