May 21, 2018 14:32 UTC
  • Russia: Marekani imekiuka mkataba wa udhibiti wa makombora

Mkuu wa idara ya kufuatilia utekelezwaji wa mikataba ya Wizara ya Ulinzi ya Russia amesema kuwa, hadi sasa Marekani imekiuka mkataba wa kudhibiti makombora uliowekwa kati ya Washington na Moscow, hasa baada ya Marekani kuunda makombora mapya ya balestiki ya masafa ya kilometa 500 hadi 5000.

Sergei Redzikov ameyasema hayo leo na kuongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni, Moscow kwa mara kadhaa imewaonya viongozi wa Marekani kutokana na hatua yao ya kupuuza mkataba huo. Kiongozi huyo wa ngazi ya juu katika Wizara ya Ulinzi ya Russia ameongeza kuwa, viongozi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wamekuwa wakitetetea hatua yao hiyo ya kuunda makombora mapya kwa kudai kuwa lengo lao ni kuifanyia majaribio mifumo ya makombora ya nchi hiyo, suala ambalo halina ukweli.

Marais wa Marekani na Russia

Mkataba wa kupunguza silaha za makombora ya masafa mafupi na ya wastani ulitiwa saini mwaka 1987 kati ya Urusi ya zamani na Marekani na kwa mujibu wa mkataba huo, makombora ya masafa ya wastani na ya masafa mafupi ya kilomita 500 hadi1000 lazima yaangamizwe. Mkataba huo ambao ulitekelezwa na serikali ya Urusi ya zamani iliyosambaratika pamoja na Marekani, uliendelea kutekelezwa hadi kufikia mwaka 1991 huku uchunguzi wake ukiendelea hadi mwaka 2001.

Kupunguzwa silaha za makombora ya masafa mafupi na ya wastani ni suala ambalo daima limekuwa likileta mvutano kati ya Marekani na Russia ambapo hivi karibuni Washington ilitangaza kwamba kutokana na Moscow kushindwa kutekeleza mkataba huo, Marekani inaiwekea vikwazo.

Tags