Wimbi la joto kali laua watu 65 nchini Pakistan
Watu wasiopungua 65 wamepoteza maisha kutokana na joto kali linaloshuhudiwa katika mji mkuu wa Pakistan, Karachi.
Anwar Kazmi, msemaji wa shirika la kibinafsi la kutoa matibabu la Edhi amesema leo Jumanne kuwa, katika kipindi cha siku nne zilizopita, chumba chao cha kuhifadhi maiti kimepokea miili 65 ya watu walioaga dunia kutokana na joto kali nchini humo.
Amesema aghalabu ya watu hao wamefariki dunia baada ya kupoteza fahamu wakiwa barabarani wanatembea.
Hata hivyo serikali ya Karachi haijathibitisha idadi ya vifo hivyo iliyotolewa na mashirika ya kibinafsi na baadhi ya vyanzo vya habari.
Kwa mujibu wa Idara ya Hali ya Hewa ya Pakistan, kiwango cha nyuzijoto nchini humo kwa sasa kimepindukia 44.
Mabadiliko ya tabianchi yamepelekea kushuhudiwa wimbi la joto kali mjini Karachi, makao makuu ya mkoa wa Sindh, ambao ulishuhudia vifo vya watu zaidi ya 1,200 kutokana na wimbi jingine la joto mwaka 2015.