Umoja wa Ulaya wapiga hatua katika kulinda biashara na Iran
(last modified Fri, 01 Jun 2018 14:03:58 GMT )
Jun 01, 2018 14:03 UTC
  • Umoja wa Ulaya wapiga hatua katika kulinda biashara na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema Umoja wa Ulaya umepiga hatua katika kuyalinda mashirika ya kibiasahra ya umoja huo ili yasilengwe kwa vikwazo vya Marekani kutokana na kufanya biashara na Iran. Hata hivyo amesema hatua zilizochukuliwa bado hazitoshi.

Akizungumza na Televisheni ya Ufaransa ya LCI, Le Drian amesema Umoja wa Ulaya umeamua kurekebisha sheria ya mwaka 1996 ambayo inauruhusu umoja huo kuyalinda mashirika ya bara hilo yasishinikizwe na Markeani kupitia vikwazo.

Amesema pamoja na kuwepo sheria hiyo, kunapaswa kuanzishwa mkakati wa kifedha wa kutotumia sarafu ya dola ya Marekani na badala yake kutumiwe sarafi nyinginezo kama vile Euro wakati wa kufanya biashara na Iran. Aidha amesema mkakti kama huo utaiwezesha Iran kuuza mafuta ghafi ya petroli pasina kutegemea sarafu ya dola.

Sheria ya mwaka 1996 ambayo Le Drian anaiashiria inalenga kuyalinda mashirika ya Umoja wa Ulaya yasiwekewe vikwazo na Marekani kutokana na kufanya biashara na Cuba au nchi zingine zinazohasimiana na Marekani.

Ikumbukwe kuwa Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Mei 8 kuwa nchi yake imejiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama JCPOA ambayo serikali iliyotangulia ya Marekani ilikuwa imeyaidhinisha. Huku akikariri matamshi yasiyo na msingi ya chuki dhidi ya Iran, Trump alisema ataiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vya nyuklia katika kipindi cha miezi mitatu hadi sita ijayo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wiki jana alibainisha masharti ya Iran kuendelea kubakia katika JCPOA na kusisitiza kuwa: "Nchi za Ulaya zinapaswa kuwasilisha azimio dhidi ya Marekani katika Baraza la Usalama, ziahidi pia kuwa kadhia za makombora na ushawishi wa Iran katika eneo hazitajadiliwa na pia zikabiliane na vikwazo vyovyote vya Marekani dhidi ya Iran." Aidha Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kununua mafuta ya Iran kwa kiwango ambacho Iran inahitaji na pia benki za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kutekeleza malipo ya kifedha kwa ajili ya biashara na serikali pamoja na sekta binafasi ya  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags