Rwanda na Russia zafanya mazungumzo kuhusu kuongeza ushirikiano wa kijeshi
Mawaziri wa mambo ya nje wa Russia na Rwanda wamefanya mazungumzo kuhusu njia za kuongeza ushirikiano wao katika masuala ya kijeshi.
Shirika la habari la Mehr limeripoti habari hiyo na kumnukuu Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia akisema baada ya mazungumzo yake na Bi Louise Mushikiwabo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda kwamba pande mbili hivi sasa zina ushirikiano wa kijeshi na kiufundi na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Rwanda vinatumia helikopta na vifaa vya usafirishaji kutoka Russia na hivi sasa mazungumzo yanaendelea baina ya pande hizo mbili kuhusu kupatiwa Rwanda mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya anga.
Lavrov ameongeza kuwa, kamati ya kimataifa ya ushirikiano wa kijeshi na kiufundi baina ya Russia na Rwanda iliundwa mwaka 2017 na kikao cha kwanza cha kamati hiyo kilifanyika mwaka huo huo mjini Kigali, Rwanda na kikao cha pili kimepangwa kufanyika mwaka huu mjini Moscow, Russia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia aidha amesisitiza kuwa, nchi hizo mbili zina mipango mizuri ya muda mrefu ya kustawisha ushirikiano wao wa kijeshi na kiufundi.
Amesema, Russia na Umoja wa Afrika zinaandaa hati ya pamoja ya ushirikiano ambayo itaongeza ushirikiano wa pande hizo mbili katika miaka ijayo.