UN: Watoto milioni 30 wamepoteza makao kutokana na vita
Takribani watoto milioni 30 wampoteza makao yao duniani kutokana na vita na sasa wanahitaji ulinzi pamoja na suluhu endelevu kwa ajili ya mustakbali wao.
Wito huo ulitolewa Jumanne na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR katika kuelekea siku ya wakimbizi duniani ambayo kila mwaka huwa Juni 20, wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kushirikisha wapenzi wa kandanda ili kuunga mkono watoto wakimbizi na wahamiaji unaojulikana kama “Nini kinachotusisimua, nini kinachotuunganisha”
UNICEF inasema idadi ya watoto milioni 30 ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote tangu vita vya pili vya dunia, na kuonya kwamba watoto hawa ambao hawajiwezi wanahitaji fursa ya kulindwa na huduma muhimu ili kuwaweka salama kwa sasa lakini pia kuhakikisha usalama wao kwa siku za usoni.
Shirika hilo pia limewataka viongozi wa dunia kuongeza maradufu juhudi zao za kuhakikisha kwamba haki, usalama na mustakbali wa watoto wasiojiweza ambao wengi wao bado wametawanywa na vita, machafuko na hali tata ya kisiasa unalindwa.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa masuala ya dharura wa UNICEF Manuel Fontaine, katika siku ya wakimbizi duniani ni muhimu kukumbuka vitisho na changamoto wanazopitia watoto wanaokimbia makwao na hasa kuondoa vikwazo vinavyofuta matumaini ya mustakabali wao.
Wakati huu ambapo kandanda imewaleta mashabiki pamoja kutoka kote duniani kwenye kombe la dunia, UNICEF ikishirikiana na wadau inatekeleza mkakati wa “Nini Kinachotusisimua, Nini Kinachotuunganisha” kwa imani kwamba endapo mapenzi ya michezo kama soka yanaweza kuvuka mipaka basi vivyo hivyo kuwaunga mkono watoto wakimbizi na wahamiaji pia kunaweza kuvuka mipaka.