MSF yalaani makubaliano ya viongozi wa Ulaya kuhusu wahajiri
Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imelaani makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Ulaya kuhusu sera za jinsi kuamiliana na wahajiri wanaoelekea barani Ulaya.
Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka imesema kuwa, nchi za Ulaya zimefikia makubaliano ambayo zaidi yamejikita katika kuzuia wahajiri kuingia barani Ulaya na kulaani operesheni za kuwaokoa wakimbizi na wahamiaji.
Miongoni mwa nukta muhimu za makubaliano ya viongozi wa Ulaya kuhusu wakimbizi ni kutoruhusu tena wimbi la wahajiri kama lile la mwaka 2015 kuelekea katika nchi za bara hilo na kuzidisha operesheni za kupambana na magenge ya kutorosha wanadamu kupitia Libya au nchi nyingine.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mjadala na mazungumzo ya masaa kadhaa baina ya viongozi wa nchi za Ulaya mjini Brussels kuhusu wahajiri haramu.
Japokuwa idadi ya wakimbizi wanaoelekea Ulaya imepungua kwa kiasi fulani lakini bado maelfu ya wahajiri na wakimbizi wanapanda mawimbi ya bahari ya Mediterrania kuelekea barani humo kwa sababu moja au nyingine.
Katika mwaka huu wa 2018 pekee wahajiri na wakimbnizi wasiopungua 785 wamefariki dunia baada ya kuzama baharini wakiwa njiani kuelekea Ulaya.