Maelfu ya Wamarekani waandamana dhidi ya sera za Trump kuhusu wahajiri
Maelfu ya watu wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya Marekani wakipinga sera na siasa za kuwapiga vita wahajiri hususan hatua ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump ya kuwatenganisha watoto wahajiri na wazazi wao.
Waandamanaji hao hususan katika miji ya Atlanta, Washington, DC na St. Louis wamesikika wakipiga nara za kupinga sera za Trump za kuwatenganisha watoto wachanga na familia zao.
Mjini Washington DC, mbali na maandamano yaliyogubika mitaa ya mji huo mkuu wa Marekani, wanaharakati wa mitandao ya kijamii wamepinga sera za kiongozi wsa nchi hiyo dhidi ya wageni na wahajiri kwa kusambaza nara ya: Wanafamilia Wanapaswa kuwa Pamoja".
Mapema vyombo vya habari vya Marekani vilitangaza kuwa, maandamano 600 yalitarajiwa kufanyika katika miji mbalimbali ya majimbo ya nchi hiyo.
Tangu Marekani ilipoanza kutekeleza sera za "ustahamilivu sifuri wa wahajiri" mwezi Mei mwaka huu, zaidi ya watoto 2300 wametenganishwa na wazazi wao na kuwekwa kwenye kambi zisizofaa. Wiki iliyopita na baada ya kushadidi malalamiko ya walimwengu dhidi ya siasa za kibaguzi za Trump, kiongozi huyo alilazimika kutupilia mbali suala la kuwatenganisha watoto na wazazi wao lakini ametoa amri washikiliwe katika vituo maalumu pamoja na wazazi wao.