Donald Tusk: Trump waheshimu washirika wa Marekani, huna marafiki wengi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46697-donald_tusk_trump_waheshimu_washirika_wa_marekani_huna_marafiki_wengi
Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya, amemtaka Rais Donald Trump wa Marekani kuwa na heshima kwa washirika wa Washington na aache kuwakosoa kila siku.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2018 23:46 UTC
  • Donald Tusk: Trump waheshimu washirika wa Marekani, huna marafiki wengi

Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya, amemtaka Rais Donald Trump wa Marekani kuwa na heshima kwa washirika wa Washington na aache kuwakosoa kila siku.

Donald Tusk, aliyasema hayo jana Jumanne kupitia ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo aliashiria ukosoaji wa kila mara wa rais huyo wa Marekani dhidi ya Umoja wa Ulaya na kusema kuwa, tabia hiyo sio sahihi kufanyiwa rafiki wa Marekani. Tusk ameongeza kwamba, ni lazima Rais Donald Trump afahamu kwamba, tofauti na kile anachokidhania yeye, hana marafiki wengi. Inafaa kuashiria kwamba, Jumanne ya jana Rais Donald Trump aliandika katika mtandao wa Twitter akiwakosoa baadhi ya wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) kwa kutoheshimu ahadi zao za bajeti katika muungano huo na kusema kuwa, mwenendo huo sio sahihi.

Rais Donald Trump wa Marekani

Mara kwa mara Trump amekuwa akiwashambulia wanachama wa muungano huo wa kijeshi kwamba hawatekelezi ahadi zao za kifedha kwa shirika hilo la kijeshi. Kikao cha Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) kinafanyika leo Jumatano mjini Brussels, Ubelgiji. Uhusiano wa Marekani na Ulaya uliharibika baada ya kikao cha kundi la G7 nchini Canada na wakati Rais Donald Trump alipowatuhumu waitifaki na washirika wa Marekani kuwa wanaitumia vibaya nchi yake katika masuala ya kibiashara. Kama hiyo haitoshi rais huyo wa Marekani amezipandishia ushuru wa asilimia 25 bidhaa za nchi za China, Mexico, Canada na Umoja wa Ulaya.